Balozi wa Comoro nchini aishukuru Serikali ya Tanzania

DAR-Balozi wa Visiwa vya Comoro nchini Tanzania, Mheshimiwa Bacar Salim ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwani kupitia Mkutano wa Tume ya Pamoja ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Comoro uliomalizika hivi karibuni, Serikali ya Tanzania imeharakisha mazungumzo na kuingia makubaliano katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na ushirikiano wa Kidiplomasia.
Dkt. Jacob G. Nduye (kushoto) Kaimu Mkurugenzi wa Kituo (CFR) akisalimiana na Balozi wa Comoro nchini Tanzania Mhe. Bacar Salim, ujumbe kutoka Comoro ,leo umetembelea Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim, jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Balozi Salim amesema haya leo wakati Ujumbe wa Comoro uliokuja hapa nchini kushiriki mkutano huo, ulipotembelea Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na kukutana na kuzungumza na Dkt. Jacob G. Nduye Kaimu Mkurugenzi kwa lengo la kujifunza na kuangalia fursa zilizopo katika masuala ya kitaaluma kati ya Tanzania na Comoro.
Bw. Abdou Nassir Madi (kushoto) Kiongozi wa Ujumbe kutoka Comoro akizungumza na Dkt. Jacob G. Nduye, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha CFR. Ujumbe kutoka Comoro umetembelea Kituo kwa lengo la kujifunza na kujadiliana kuhusu fursa zilizopo baina ya Tanzania na Comoro.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuingia makubaliano yenye faida kwa pande zote mbili, mazungumzo yalienda haraka na uamuzi ukafikiwa mapema tunashukuru. Comoro na Tanzania tuna Undugu, Ujirani, Urafiki na Wacomoro wanapokuja Tanzania wapo nyumbani,” amesema Mheshimiwa Balozi Salim.

Akizungumza wakati wa majadiliano, Kaimu Mkurugenzi Dkt Jacob G. Nduye ameushukuru ujumbe kutoka Comoro kwa kuamua kukitembelea Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na amesema Kituo kinatoa mafunzo ya muda mfupi, muda mrefu na programu maalum katika masuala ya Uhusiano wa Kimataifa, Diplomasia, Ulinzi na Usalama, Stadi za Stratejia, Lugha mbalimbali na kufanya utafiti.
Balozi wa Comoro nchini Tanzania, Mhe. Bacar Salim (kulia), akiwa na Bw. Faicoil Mohamed Djitihadi, Mkurugenzi wa masuala ya Siasa na Sheria na Bw. Hassane Oumair, Mtaalam wa Sheria kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wakishiriki mazungumzo kuhusu fursa zilizopo kati ya Tanzania na Comoro.
Dkt. Jacob G. Nduye (aliyekaa katikati) Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha CFR akiwa katika picha ya pamoja na Ujumbe kutoka Comoro na baadhi ya Wakuu wa Idara na Vitengo wa Kituo cha CFR mara baada ya mazungumzo.

Kwa upande wa fursa, Dkt. Jacob G. Nduye amesema kupitia majadiliano yaliyofanyika miongoni mwa fursa zilizopo kwa pande zote mbili kati ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na Vyuo vya Elimu ya juu vilivyopo nchini Comoro ni kubadilishana wataalam, programu za mafunzo na lugha mbalimbali.

Ujumbe wa Comoro umeongozwa na Bw. Abdou Nassir Madi, Mkurugenzi Mkuu wa Biashara na Waziri wa zamani wa Uchumi wa Comoro; Bw. Faicoil Mohamed Djitihadi, Mkurugenzi wa Masuala ya Siasa na Sheria na Bw. Hassane Oumair, Mtaalam wa Sheria, Idara ya Sheria kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Comoro.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news