KATAVI-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ameeleza kuwa Serikali inaendelea kuboresha miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Katavi ambapo sasa barabara ya kutoka Tabora hadi Mpanda (km 352) ni ya kiwango cha lami.
Rais Dkt. Samia ameeleza hayo leo Julai 13, 2024 wakati akizungumza na wananchi wa Inyonga Wilayani Mlele wakati wa ziara yake mkoani Katavi.
“Wakati nimekuja kipindi cha kampeni kutoka Tabora kwenda Mpanda ilikuwa ni vumbi tupu lakini leo nimeteleza mpaka nimesinzia, Barabara ni nzuri na ni maendeleo makubwa sana, niwapongeze sana,"amesema Dkt. Samia.
Dkt. Samia ameeleza miradi mingine inayoendelea kutekelezwa na Serikali katika Mkoa wa Katavi ni pamoja na ujenzi wa barabara ya Kibaoni - Makutano ya Mlele (km 50), Vikonge - Luhafwe (km 25), Luhafwe - Mishamo (km 37) na Kagwira - Karema (km 110) kwa kiwango cha lami.
Aidha, Dkt. Samia ameeleza kuwa pamoja na miradi inayoendelea kutekelezwa, Serikali ipo katika hatua za kutafuta Makandarasi wa kutekeleza miradi mingine ya miundombinu ya barabara katika Mkoa wa Katavi.
Ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi kutunza na kulinda miundombunu ya Barabara iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa.
Tags
Barabara mkoani Katavi
Dr Samia Suluhu Hassan
Habari
Sekta ya Ujenzi Tanzania
TANROADS Tanzania
Wizara ya Ujenzi Tanzania