Benki Kuu ya Tanzania (BoT) yapongeza uanzishwaji wa kiwanda kipya cha mbolea Itracom Fertilizer Ltd

DODOMA-Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepongeza uanzishwaji wa kiwanda kipya cha mbolea cha Itracom kilichopo jijini Dodoma ambacho kinatarajiwa kuwa na uwezo wa kuzalisha tani milioni moja za mbolea ifikapo mwezi Agosti mwaka huu, ikiwa ni ziada ya tani 400,000 za mahitaji ya nchi kwa sasa.Akizungumza wakati wa ziara ya BoT kiwandani hapo, kiongozi wa msafara wa Benki Kuu, Kaimu Mkurugenzi wa Utafiti na Sera za Uchumi, Bw. Lekinyi Mollel, alisema kuwa uwekezaji mkubwa uliofanywa katika kiwanda hicho utasaidia nchi kujitosheleza kwa mbolea na kupunguza matumizi ya fedha za kigeni kuagiza pembejeo hiyo muhimu kutoka nje.

“Kuanzisha kiwanda hiki cha Itracom kunachochea fursa za kiuchumi na kuokoa fedha za kigeni zinazotumika kuagiza mbolea toka nje ya nchi," amesema Bw. Mollel.

Lengo la ziara hiyo ya Benki Kuu ni kujifunza mazingira ya kazi, mazingira ya uwekezaji, masuala ya masoko na mipango endelevu ya kiwanda.
“Tumefika, tumeona na tunajua kinachoendelea. Tunajifunza jinsi kiwanda kilivyojipanga kusaidia uchumi wa nchi na kuokoa uagizaji wa mbolea toka nje kwa kuzalisha hapahapa nchini,"amesema Bw. Mollel.

Awali, akizungumza na ujumbe wa Benki Kuu, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Itracom Fertilizer Ltd, Dkt. Kenneth Machuki, alisema kuwa, “Hadi hivi sasa tuna uwezo wa kuzalisha tani laki sita (600,000), wiki ijayo tutaongeza uwezo wa kuzalisha tani 200,000 zingine na ifikapo mwezi Agosti mwaka huu tutafikia malengo yetu ya kuweza kuzalisha tani milioni moja kwa mwaka.”
Kwa uzalishaji huo, Dkt. Machuki alisema Bodi ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) inakadiria matumizi ya mbolea nchini kwa mwaka kuwa ni tani laki sita, hivyo kutakuwa na ziada ya tani 400,000 za kuuza nje.

Kiwanda hicho ambacho muwezekezaji anatoka nchini Burundi, ni kikubwa na cha aina yake na kinatarajiwa kuiwezesha Tanzania kutimiza lengo la kutoagiza kabisa mbolea kutoka nje ya nchi ifikapo mwaka 2030.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news