NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI
WAZIRI Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa amepokea mchango wa shilingi 3,170,000/= wa madereva bodaboda nchini, walioutoa kwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassani kwa ajili ya kumuwezesha kuchua fomu ya kugombea urais mwaka 2025 baada ya kuridhishwa na uongozi wake.
Mhe. Mchengerwa amepokea mchango huo katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salam, wakati akizindua sare maalum (uniform) na mfumo wa kidijitali (kanzidata) wa madereva Bodaboda na bajaji wa jiji la Dar es Salaam.
“Leo nimeshuhudia na kupokea mchango wenu wa kumuwezesha Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuchukua fomu ya kugombea urais mwaka 2025 kwa mapenzi yenu wenyewe, bila kushurutishwa na hii ni kwasababu Rais Samia ameingia katika mioyo yenu na watanzania wengine kutokana na uongozi wake imara,” Mhe. Mchengerwa ameeleza.
Mhe. Mchengerwa amesema, uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan umegusa mioyo ya madereva boda boda, wakulima, wafanyakazi na kila mtanzania, hivyo kila mmoja kwa nafasi yake ana sababu ya kumuunga mkono kwa vitendo kwa kumchangia ili aweze kutimiza azma yake ya kuendelea kuliongoza taifa na kuliletea maendeleo.
Waziri Mchengerwa amewapongeza viongozi wa boda boda kutoka katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tanga, Mwanza, Geita, Katavi, Iringa, Mbeya, Songwe, Rukwa, Lindi,Tabora, Dar es Salaam pamoja na Zanzibar kwa kuwasilisha michango yao ya kumuwezesha Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuchukua fomu ya kuombea urais mwaka 2025.
“Fedha hizi 3,170,000/= mlizo changa na kunikabidhi, nami leo hii hii nitakwenda kuzikabidhi kwa Mhe. Rais ili atambue namna ambavyo mna muunga mkono kutokana na kuthamini uongozi wake madhubuti na imara,” Mhe. Mchengera amesema.