BoT yaendelea kutoa elimu Maonesho ya Sabasaba, Gavana Tutuba awatembelea

DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, ametembelea banda la BoT kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere Barabara ya Kilwa, Temeke, jijini Dar es Salaam.
Katika maonesho hayo, BoT inatoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake, ambapo wananchi wanapata fursa ya kujifunza mambo mbalimbali ikiwemo sera za fedha, namna ya kuwekeza katika dhamana za serikali, mifumo ya malipo ya taifa, na namna BoT inavyosimamia sekta ya fedha nchini.
Vilevile, BoT inaelimisha umma kuhusu utatuzi wa malalamiko ya mtumiaji wa huduma za kifedha, masuala ya ajira na utumishi Benki Kuu, pamoja na nafasi za masomo katika Chuo cha BoT na Bodi ya Bima ya Amana.

Pia, BoT inatoa elimu kuhusu utambuzi wa alama za usalama katika noti za Tanzania na njia sahihi za utunzaji wa noti na sarafu. Wananchi wanaotembelea banda la BoT wanapata fursa ya kuona na kujifunza kwa vitendo alama hizi muhimu zinazosaidia kutambua noti halali za Tanzania.
Ushiriki wa BoT katika Maonesho ya Sabasaba umewezesha kuwasiliana moja kwa moja na wananchi, kutoa ufafanuzi kuhusu masuala ya kifedha, na kujibu maswali yanayohusiana na kazi za Benki Kuu.

Jitihada hizo za BoT zinachangia kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya kifedha na kuwajengea uwezo wa kufanya maamuzi sahihi ya kifedha, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza sekta ya fedha na uchumi wa nchi kwa ujumla.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news