NA GODFREY NNKO
BENKI Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuendelea kwa ukomo wa riba ya asilimia 6 katika robo ya tatu ya mwaka 2024 kati yake na benki za biashara nchini.
Riba hiyo itatumika katika kipindi cha robo ya tatu kuanzia leo Julai 4,2024 hadi Septemba, mwaka huu.
Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Sera za Uchumi na Fedha), Dkt. Yamungu Kayandabila kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ametangaza riba hiyo leo Julai 4,2024 katika ofisi za makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam.
"Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania, imeamua Riba ya Benki Kuu (CBR) kuendelea kuwa asilimia 6 kwa robo mwaka itakayoishia Septemba 2024.
"Uamuzi huu umefikiwa katika kikao cha Kamati kilichofanyika tarehe 3 Julai 2024. Tathmini ya kamati kuhusu mwelekeo wa uchumi na vihatarishi mbalimbali inaonesha kwamba,utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa kipindi cha Januari hadi Juni, 2024 umefanikiwa kudhibiti mfumuko wa bei na kubaki chini ya lengo la asilimia 5.
"Maamuzi ya kamati pia yanazingatia mtazamo chanya wa uchumi wa dunia, ambapo matarajio ni kuendelea kupungua kwa mfumuko wa bei katika nchi nyingi, kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani, na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia.
Aidha, Kamatii natarajia uchumi wa ndani kuendelea kukua kwa kasi, sanjari na upatikanaji wa chakula cha kutosha, na kupungua kwa kasi ya kushuka kwa thamani ya shilingi kufuatia ongezeko la mapato ya fedha za kigeni kutokana na shughuli za utalii, pamoja na mauzo ya dhahabu na mazao ya biashara na chakula."
Hayo yanajiri ikiwa utekelezaji wa Sera ya Fedha kwa kutumia Mfumo wa Riba ya Benki Kuu (Central Bank Rate) ulianza Januari 19, 2024 ambapo BoT iliachana na mfumo uliokuwepo wa Ujazi wa Fedha.
Katika robo ya kwanza ukomo wa riba ulikuwa asilimia 5.5 kati ya BoT na benki za biashara ili kudhibiti mfumuko wa bei na kuchochea ukuaji wa uchumi nchini.
Aidha, robo ya pili ambayo ilikuwa mwezi Aprili hadi mwishoni mwa Juni, mwaka huu ukomo wa riba ulikuwa asilimia 6.
Naibu Gavana Dkt. Kayandabila amesema, maamuzi ya kamati yanazingatia mtazamo chanya wa ukuaji wa uchumi duniani.
Vile vile, Naibu Gavana Dkt.Kayandabila amesema, katika kutathmini mwenendo wa uchumi wa Dunia, kamati ilibaini kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika nchi nyingi kwa robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2024.
Pia,mfumuko wa bei umeendelea kupungua, sanjari na kuimarika kwa ukwasi katika masoko ya fedha duniani, na benki kuu katika nchi nyingi kuanza kupunguza viwango vya riba.
"Bei ya mafuta ghafi ilipungua, licha ya kuongezeka kidogo mwishoni mwa mwezi Juni 2024. Bei ya dhahabu iliendelea kuwa juu, ikiashiria dhahabu kuendelea kutumika kama uwekezaji mbadala katika mazingira ya kushuka kwa thamani ya sarafu mbalimbali na migogoro ya kisiasa duniani."
Amesema,matarajio ni uchumi wa dunia kuendelea kuimarika katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2024 na 2025, licha ya kuwepo kwa hatari ya kuongezeka kwa migogoro ya kisiasa na mizozo ya kibiashara.