GEITA-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Bukombe mkoani Geita, Mhe. Dkt. Doto Biteko amemshukuru Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa heshima kubwa aliyowapa Watu wa Bukombe kwa kuwaletea Maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Amesema hayo wakati akihutubia mkutano wa wa hadhara katika Uwanja wa Lyambamgongo Center iliyopo Kata ya Lyambamgongo, Jimbo la Bukombe mkoani Geita.
“Nataka niwambieni mambo mazuri yanakuja, Mama Samia amesema anataka aione Bukombe mpya na mimi nawahakikishieni itabadilika Lyambamgongo haikuwa hivi na ninyi ni mashahidi lakini Rais wetu ametuletea huduma mbalimbali za maendeleo na leo tumepata barabara ya kutoka Lyambamgongo hadi Ifunde, Ishoro, Nyamakungu, hatukuwa na Zahanati leo tumepata Zahanati na Nishati ya umeme wa uhakika mambo mazuri zaidi yanakuja na Bukombe itabadilika,”amesisitiza Dkt. Biteko.
Dkt. Doto Biteko amewataka wananchi wa Kijiji cha Lyambamgongo na Jimbo la Bukombe kwa ujumla kujiandaa kwa ajili ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika mwaka huu kwa kuchagua viongozi wenye sifa watakaosaidia kuleta maendeleo.
“Muda utakapofika tuwe tayari kwaajili ya kujiandikisha katika Daftari la kupiga kura ili tuweze kuchagua viongozi wazuri wenye sifa za kuchaguliwa ambao watasaidia kuleta maendeleo, tunataka jimbo la Bukombe libadilike kwa kuwa na watu wenye maono au mawazo mazuri yatakayosaidia utatuzi wa changamoto zinazotukabili,”amefafanua na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo jimboni humo.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko amesema kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan atafanya ziara mkoani Geita na kuwasalimia wa Bukombe kwa kuwa anataka kuona miradi mingi inatekelezwa na hivyo yeye kama Mbunge ataendelea kuhakikisha maendeleo ya kweli yanaenda kwenye maeneo ya wananchi.Naye, Diwani wa kata ya Lyambamgongo, Mhe. Bonifasi Shitobelo amesema hapo awali huduma zilikuwa mbali na gharama za kwenda kupata matibabu zilikuwa juu lakini sasa Serikali imesogeza huduma kwa wananchi.
"Tunaishukuru Serikali na mbunge wetu Mhe. Doto Biteko kwa kuwezesha ukamirishaji wa ujenzi wa Zahanati, Barabara ya kutoka Lyambamgongo hadi Ifunde na Shule ya Msingi katika jimbo la Bukombe."
Naye, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Geita, Bw. Nicholaus Kasendamila amemshukuru Dkt. Biteko kwa kuendelea kuwasaidia wananchi wa Bukombe kwa kuhakikisha wanapata maendeleo kwa kuwa na miradi mbalimbali.
Aidha, amewasihi wananchi wa Bukombe kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa “Huu ni mwaka wa uchaguzi tunatakiwa kujiandaa na viongozi wa CCM katika Mkoa huo tuhamasishe wapiga kura kushiriki katika uchaguzi na hatimaye kuchagua viongozi wazuri”.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Mhe. Mhe. Stanslaus Nyongo amesema kuwa Mbunge anaefanya kazi vizuri anatangaza Jimbo łake na leo hii Dkt. Doto Biteko ameendelea kulitangaza vema jambo hilo kwa kazi nzuri anayoifanya katika Jimbo la Bukombe.