Chonji wenzake wahukumiwa maisha jela kwa dawa za kulevya

DAR-Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, imewahukumu kifungo cha maisha jela washtakiwa watano baada ya kutiwa hatiani kwa makosa ya kusafirisha dawa za kulevya aina za Heroine gramu 5,309.57 na Coceine zenye uzito wa gramu 894.28.

Hukumu hiyo imetolewa Julai 11, 2024 na Jaji Awamu Mbagwa, aliyesikiliza kesi hiyo ya jinai namba 58/2023.
Waliohukumiwa ni Muharami Abdallah, maarufu Chonji, Abdul Chumbi, Rehan Umande, Tanaka Mwakasafule na Maliki Maunda.

Baada ya kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, Jaji Mbagwa aliwahukumu kifungo cha maisha jela washtakiwa wote watano akieleza upande wa mashitaka umethibitisha makosa hayo bila kuacha shaka yoyote.

Washtakiwa walidaiwa kusafirisha dawa za kulevya kinyume cha kifungu cha 16 (1) (b) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.

Katika shitaka la kwanza, walidaiwa Oktoba 21, 2014 eneo la Magomeni Makanya, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, walisafirisha dawa za kulevya aina ya Heroine ambazo iwapo zingeuzwa zingekusanya kiasi fulani cha fedha.

Shtaka la pili, walidaiwa siku hiyo hiyo na katika eneo hilo, walisafirisha dawa za kulevya aina ya Cocaine zenye thamani fulani ya fedha.

Katika kesi hiyo upande wa mashitaka uliwakilishwa na mawakili watano wakiongozwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Saraji Iboru, huku washtakiwa wakitetewa na mawakili wanane wakiongozwa na Juma Nassoro.

Upande wa mashitaka ulikuwa na mashahidi 10 na vielelezo 12, ikiwamo mizani tatu za kupimia, bastola aina ya Browing iliyokuwa na risasi nane, ripoti ya mkemia, simu, cheti cha kukamata na ripoti ya kitaalamu ya taarifa ya uchunguzi na uthibitisho wa picha mjongeo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news