DAR-Mchezaji wa Kimataifa ambaye ni raia wa Zambia, Clatous Chota Chama anayecheza katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara, baada ya kuitumikia Klabu ya Simba ya jijini Dar es Salaam kwa miaka sita, ameaga rasmi huku akishukuru kwa mafanikio tele.
Chama ameyabainisha hayo leo Julai 3,2024 baada ya kumaliza mkataba wake wa kuichezea Simba SC tangu Juni 30, 2024 na kisha Julai Mosi,2024 akatambulishwa rasmi kama mchezaji mpya wa Yanga SC ya jijini Dar es Salaam.
Nyota huyo alijiunga Simba SC kwa mara ya kwanza mwaka 2018 akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia na kisha 2021 kuondoka Simba SC na kujiunga na RS Berkane aliyodumu kwa msimu mmoja na kurejea Simba SC mwaka 2022.
Amesema,miaka sita iliyopita alifika Simba kama mgeni na klabu hiyo ikamfanya kuwa bora zaidi ya alivyokuwa kabla.
Vile vile akawa sehemu ya watu walioitawala ardhi na kuifanya Simba kupanua zaidi himaya yake hadi sehemu nyingine barani Afrika.
"Hakuna mtu anayeweza kubadilisha historia tuliyotengeneza pamoja.Wanasema shoo haijaisha mpaka mwanamke mnene aimbe na ninaamini huu wimbo utawapatia thamani ya muda wenu, nawatakia kila la kheri, tutaendelea kuonana, nguvu moja.”