PWANI-Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani, Mheshimiwa Petro Magoti amepiga marufuku pikipiki kubeba mkaa ndani ya wilaya hiyo.
Marufuku hiyo inaanzia leo Julai 10,2024 na atakayekamatwa atalipa faini ya shilingi milioni moja na asipolipa faini hiyo pikipiki itataifishwa.
Vile vile, Mheshimiwa Magoti pia amepiga marufuku magari yenye mkaa kutembea wilayani Kisarawe kuanzia saa 12 jioni na atakayekaidi gari lake na mkaa vitakamatwa kwa hatua zaidi.
“Sasa naomba nitoe maelekezo, kwa sheria za nchi yetu kote nchini ni marufuku pikipiki kubeba mkaa kwa sheria za LATRA zipo sio sheria za Magoti wala za DC.
"Nipo kusimamia sheria, ni marufuku pikipiki kubeba mkaa katika Wilaya ya Kisarawe, nikikukamata faini ya pikipiki ni milioni moja na kuna muda tukiikamata pikipiki usipotoa faini tunataifisha pikipiki;
Ameyasema hayo leo Julai 10,2024 wakati akiwa kwenye kikao cha Kamati ya Uvunaji Wilaya kilichohusisha wajumbe zaidi ya 30 kutoka vijiji vyote vilivyozungukwa na misitu.
“Agizo namba mbili kisheria mwisho gari lenye mkaa kutembea kwenye barabara ndani ya Wilaya ya Kisarawe ni saa 12 jioni mwisho, ukizidisha gari tunalikamata kisha utalipa faini milioni moja ukishindwa tunachukua gari na mkaa.
"Muda uliopewa kulipa faini ukipita tunataifisha gari na mkaa, naelekeza kamata gari la mtu yoyote ambalo limevunja sheria iwe gari la kiongozi, mfanyabiashara au mtumishi likikamatwa tutafuata sheria,”amesisitiza Mheshimiwa Magoti.
Ameongeza kuwa, kwenye vikao mbalimbali alisema ikifika Julai,2024 wanaanza kusimamia sheria, kanuni na taratibu.
Pia, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan alitoa maelekezo nchini kuhusu kupunguza matumizi ya mkaa badala yake wanatumia nishati safi ya kupikia ambayo inajumuisha gesi.
"Misitu ni mali na sisi Kisarawe tuna bahati ya kuwa na mapori mengi ya misitu.”