DCEA yamdaka 'mpishi' wa dawa za kulevya huko Kilimani Manzese

NA GODFREY NNKO

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) inamshikilia, Bw.Shaban Musa Adam mwenye umri wa miaka 54 mkazi wa Dar es Salaam kwa tuhuma za kutengeneza dawa za kulevya.
Hayo yamesemwa leo Julai 17,2024 jijini Dar es Salaam na Kamishna Jenerali wa mamlaka hiyo, Aretas Lyimo wakati akizungumza na wanahabari kupitia hafla fupi ambayo imejumuisha tukio la kuwapa tuzo wadau mbalimbali.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, mtuhumiwa alikamatwa Juni 11,2024 nyumbani kwake huko Kilimani Manzese akitengeneza dawa za kulevya ambazo alizitambulisha kama Heroine.

"Alikuwa anazitengeneza kwa kutumia dawa tiba zenye asili ya kulevya akichanganya na kemikali bashirifu.

"Baada ya kutengeneza dawa hizo husafirishwa kwa kutumia mabasi ya abiria kama vifurushi kwenda mikoa mbalimbali nchini."

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, mtuhumiwa huyo aliieleza mamlaka hiyo kuwa siku za nyuma alikuwa akitengeneza dawa hizo nchi za Bara la Asia katika magenge ya wazalishaji wa dawa za kulevya.

Vile vile amesema, mtuhumiwa alitumika kama mbebaji wa dawa hizo ambapo baada ya kurejeq nchini aliendelea kutekeleza uhalifu huo hapa Tanzania.

"Dawa hizi zinaweza kusababisha madhara makubwa kiafya kwa mtumiaji kama magonjwa ya moyo, ini, figo, mfumo wa hewa, saratani yakiwemo magonjwa ya akili na uraibu.

"Mbinu hii imekuwa ikitumiwa baada ya dawa za kulevya aina ya Heroine na nyinginezo kuadimika mtaani, Serikali imebaini na kuchukua hatua na tunaendelea kufuatilia mtandao wa uhalifu huo.

"Kwa hiyo, huyu mtengenezaji kwa sababu mara nyingi tumekuwa tukikamata dawa za kulevya, tunavyopeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali tunakuta kuna mchanganyiko wa dawa tiba zenye asili za kulevya na hizi kemikali bashirifu.

"Na hii imetokea kutokana na operesheni kubwa tulizozifanya hapa nchini kwa kukamata wasafirishaji wakubwa wa dawa za kulevya ambao walikuwa wanasafirisha hizo dawa kutoka mataifa mbalimbali kuziingiza hapa nchini.

Baada ya kukata hii mitandao ya wafanyabiashara wa dawa za kulevya kukawa na uadimu wa hizi dawa za kulevya.

"Kwa hiyo, akaibuka huyu akawa sasa anatengeneza hizo dawa kupitia nyumbani, anachanganya vitu mbalimbali ikiwemo hizo kemikali bashirifu, lakini mbaya zaidi anatumia dawa tiba zenye asili ya dawa za kulevya ikiwemo dawa zinazotibu kansa, dawa zinazotibu maumivu makali na dawa zinginezo anachanganya na vifaa vingine anapata Heroine.

"Na mara nyingi hizi ndizo zinazouzwa kwenye miji mikubwa sasa hivi. Kwa hiyo, hizi dawa feki za Heroine ndizo zinazouzwa kwenye maeneo mbalimbali na ndio maana pia kumeibuka vifo vya ghafla vya wale watumiaji wa dawa za kulevya kutokana na hizi dawa na mchanganyiko wake kiafya zinaathari kubwa sana.

"Lazima Watanzania wote tushirikiane kukomesha hili jambo ndiyo maana tumemkamata huyu mtengenezaji hivyo tumekata cheni kubwa sana. Kwani alikuwa anatusumbua hapa nchini kwa kutengeneza dawa za kulevya."

Pia, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, kemikali bashirifu walizokamata ambazo mtuhumiwa huyo alikuwa akizitumia kutengeneza dawa za kulevya zimeisha muda wake.

"Kwa hiyo zinazidi kuleta madhara makubwa katika mwili wa binadamu pale anapotumia hizo dawa za kulevya."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

2 Comments

  1. Huyu Jamaa aliona aanzishe kiwanda chake badala yakufaidisha wengine kwakuwabebea tuuu

    ReplyDelete
  2. Huyu Jamaa aliona aanzishe kiwanda chake badala yakufaidisha wengine kwakuwabebea tuuu

    ReplyDelete
Previous Post Next Post

International news