NA GODFREY NNKO
KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo amesema,mamlaka hiyo inathamini na kutambua ushirikikiano unaotolewa na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, wananchi na mamlaka nyingine za udhibiti katika kupambana na kudhibiti tatizo la dawa za kulevya nchini.
Sambamba na wadau wa vyombo vya habari nchini ambao wamekuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii kuhusu mapambano dhidi ya dawa za kulevya nchini.
Kamishna Jenerali Lyimo ameyasema hayo Julai 17,2024 jijini Dar es Salaam wakati akitoa tuzo kwa wadau mbalimbali ambao wameendelea kushirikiana bega kwa bega na mamlaka katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Tuzo ya kwanza ilitolewa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ambapo Kamishna Jenerali Lyimo amesema, mamlaka hiyo inatambua mchango wake katika kuratibu upelelezi na uendeshaji wa mashtaka ya dawa za kulevya.
Aidha, tuzo ya pili ilitolewa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali ambaye amekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) nayo ilikabidhiwa tuzo kwa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Vile vile, Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ilikabidhiwa tuzo na mamlaka hiyo kwa kutambua mchango wake katika kuzuia na kupambana na dawa za kulevya nchini.
Akipokea tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi amesema hospitali hiyo ilianzisha kliniki ya Methadhone mwaka 2011 ikiwa ni ya kwanza nchini ili kutoa huduma kwa warahibu wa dawa ya kulevya aina ya afyuni waweze kuondokana na tatizo hilo.
Prof. Janabi amesema, tangu kuanzishwa huduma hiyo hadi kufikia Juni 2024 jumla ya warahibu 3,840 wameandikishwa kupata huduma ya methadone wanaume wakiwa 3,692 na wanawake 148 ambapo warahibu 900 wanaohudumiwa kila siku kunywa dawa ya methadone kati yao wanawake ni 30.
Tuzo nyingine ilitolewa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga kutokana na jitihada zake za kuimarisha mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Nyingine imetolewa kwa ITV kwa kutoa mchango mkubwa katika kuhabarisha umma na kurusha matangazo katika kilele cha Maadhimisho ya Kitaifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya Duniani ambayo kwa mwaka huu yamefanika jijini Mwanza.
Wengine ni THPS, ICAP, TANPUD, TOGT, Pili Missanah Foundation, Mohamed Bucck, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na Railway Children Limited.
Akikabidhi tuzo hizo kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan, Kamishna Jenerali Lyimo amesema, mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wote ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha Tanzania inabaki salama bila dawa za kulevya.