Dira ya Maendeleo ni Mali ya Watanzania-Prof.Mkumbo

NA ADELINA JOHNBOSCO
Maelezo

WATANZANIA wametakiwa kushiriki kikamilifu katika zoezi la kutoa maoni yatakayowezesha kuandaliwa kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, amesema hayo Julai 27,2024 wakati akihutubia wananchi waliohudhuria Kongamano la wadau na wananchi wa Kanda ya Kaskazini, kuhusu ukusanyaji wa maoni ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, lililofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).

Akisisitiza, Waziri Mkumbo amesema, "kuna watu kwa kujua ama kutojua wanadhani kwamba, Dira ya Taifa ni kwa ajili ya viongozi walioko kwenye nafasi mbalimbali Serikalini, dhana hii si kweli, Dira ya Taifa ni mali ya Watanzania wote, hivyo kila mmoja wetu atoe maoni ili tupate Tanzania tunayoitaka kwa miaka 25 ijayo."

Sambamba na hayo, Waziri Mkumbo amewakumbusha Watanzania kwamba, maendeleo tuliyonayo hivi sasa, ni zao la Dira ya miaka 25 inayomalizika iliyokuwa ikijulikana kwa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025, hivyo amewataka wananchi kutoa maoni ili Serikali iweze kuyachukua na kuyafanyia kazi kwa ajili ya kuwa na maendeleo zaidi ya yaliyopo kwa sasa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Batilda Burian, akiongea kwa niaba ya Wakuu wa mikoa wenzake wa Kanda ya Kaskazini, amesema wanamshukuru Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuelekeza ushiriki wa wananchi katika kupata Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

"Tumeweza kuona uimarishwaji wa miundombinu katika sekta mbalimbali, uboreshwaji na ujenzi wa barabara hasa za vijijini, tumeona uanzishwaji na uboreshaji wa taasisi mbalimbali ikiwemo TASAF iliyoboresha huduma za kijamii katika mikakati ya kuondoa umaskini nchini, hii yote ni matunda ya Dira 2025," ameongeza Balozi Burian.

Kongamano hilo pia limehusisha zoezi la wananchi wa Kanda ya Kaskazini waliohudhuria kushiriki kutoa maoni yao mbele ya viongozi mbalimbali waliokuwepo kuhusu mtazamo wao wa Tanzania waitakayo itakayopatikana kutoka kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050. Mikoa inayounda Kanda ya Kaskazini ni mkoa wa Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Tanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news