SONGWE-Mkurugenzi wa Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Dkt. Rashid Mfaume ameshauri Halmashauri ya Mbozi mkoani Songwe kufanya matengenezo ya gari la Idara ya Afya iliyoegeshwa kwa takribani miaka miwili bila taarifa rasmi ya ubovu wa gari hilo.
Dkt. Mfaume ametoa ushauri huo kwenye ziara ya usimamizi shirikishi, ufuatiliaji na ukaguzi wa miundombinu ya afya katika mkoa huo akiwa ameambatana na timu ya Afya,Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI.
Ni baada ya kutembelea maegesho ya magari katika ofisi za Halmashauri hiyo na kukuta gari namba DFP 9647 la idara ya Afya limeegeshwa kwa muda mrefu.
“Tunalalamika tunashida ya magari, kwa nini yaliyopo hatuyatengenezi haiwezekani miaka yote mko hapa na hamjui hii gari inashida gani, mmeamua kuipaki mnatengeneza mazingira ya kuuziana wakati sisi watumishi wa Idara ya Afya tuna changamoto ya magari na hapa."
"Tunatoa maelekezo tunataka hii gari (DFP 9647) itengenezwe na tungependa tupate taarifa wiki ya pili ya mwezi wa saba tupatiwe ‘video clip’ kwamba hii gari iko barabarani inatumika kusambazia chanjo na usimamizi shirikishi hatuwezi kuwa na magari yamepaki halafu mnasema mna shida ya magari wakati yaliyokuwepo hamyatengenezi,” amesema.
Katika kusisitiza hilo, amezitaka timu za usimamizi wa shughuli za Afya za Halmashauri (CHMT) na mkoa (RHMT) nchini kufuatili taarifa za magari ya idara ya Afya ambayo yameegeshwa kwa madai ya uharibufu wa kawaida waombe wakurugenzi wa Halmashauri kuyafanyia marekebisho ili shughuli za usimamizi na ufuatiliaji wa huduma za Afya zifanyike kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Abdallah Nandonde ameahidi kufanya marekebisho hayo na gari hilo litaanza kufanya kazi za ufuatiliaji na usimamizi wa shughuli za afya.