Gavana Tutuba,Balozi Ismail wajadiliana kuhusu sekta ya fedha na uchumi

DAR-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba,tarehe 23 Julai, 2024 amekutana na Balozi wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri nchini Tanzania, Mhe. Sherif Ismail, na kujadiliana masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya fedha na uchumi kiujumla.Akizungumza katika mkutano huo, Gavana Tutuba amesema Benki Kuu ya Tanzania itaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati yake na Benki Kuu ya Misri pamoja na Serikali ya nchi hiyo kupitia programu mbalimbali za kukuza uchumi baina ya nchi hizo.
Amesema, takwimu zinaonesha kuwa biashara kati ya Tanzania na Misri imeendelea kuimarika kutokana na mahusiano mazuri ambayo yamedumu kwa muda mrefu baina ya nchi hizi mbili.
Ameongeza kuwa, uwepo wa wawekezaji wengi kutoka Misri hapa nchini ni chachu ya kuvutia wawekezaji wengine kutoka nchini humo kutokana na fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo Tanzania.
Aidha, Gavana Tutuba ameueleza ujumbe huo wa Ubalozi wa Misri nchini kuwa Serikali kupitia Benki Kuu imekuwa ikikaribisha wawekezaji mbalimbali wa sekta ya mabenki kuja kuwekeza kwenye sekta hiyo kutokana na utulivu wa sekta ya fedha na mazingira rafiki ya uwekezaji nchini.
Kwa upande wake, Balozi Sheriff Ismail, ameipongeza Benki Kuu kwa mchango wake katika kusimamia uchumi wa nchi na ameahidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutekeleza programu mbalimbali zenye manufaa ya kiuchumi kwa nchi zote mbili.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news