DODOMA-Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imepokea taarifa ya Utafiti wa Madini ya Dhahabu unaofanywa na Kampuni ya Twiga Corporation Limited inayomilikiwa kwa ubia kati ya Serikali kwa asilimia 16 na Kampuni ya Barrick Tanzania Limited kwa asilimia 84 ikiwa ni utaratibu kwa Serikali kupokea taarifa za maendeleo ya utafiti kutoka kwa kampuni za uchimbaji madini kila baada ya Robo Mwaka.

Naye, Mjiolojia mwandamizi kutoka GST Bw. Muhudi Ngerezi ametoa wasilisho kuhusu historia ya GST, kazi zinazo tekelezwa na taasisi hiyo ikiwemo shughuli za utafiti wa njia ya Jiolojia, Jiofizikia, Jiokemia na kuelezea shughuli za maabara zinazofanywa na taasisi hiyo.
Aidha, Meneja wa Sehemu ya Jiolojia Bw. Maswi Solomon akitoa neno la shukrani la kuhitimisha amesema GST ndiyo kitovu cha taarifa za tafiti za madini nchini ikiwemo kuzihakiki hivyo ameisihi Kampuni ya Barrick kuendelea kutoa taarifa za utafiti zinazofanywa na Kampuni hiyo kila baada ya Robo Mwaka kama Sheria ya Madini inavyowataka.
Huku akisema kazi hiyo inairahisishia GST kuzihakiki kwa kuwa mambo mengi yenye dukuduku yanakuwa yanatolewa ufafanuzi wakati wa wasilisho.
Pamoja na mambo mengine, Meneja wa Utawala na Rasilimaliwatu wa GST Jacqueline Kaluwa ameiomba Kampuni ya Barrick kuwapa fursa Wataalamu kutoka GST kujifunza teknolojia mbalimbali za utafiti kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji kazi wa Wataalamu hao hasa kwenye nyanja ya ukadiriaji mashapo.
