Halmashauri tambueni jukumu la kusafisha barabara na mitaro-Mhandisi Mativila

DODOMA-Serikali imezitaka Halmashauri zote nchini kutambua kuwa jukumu la kusafisha barabara na mitaro ni la kwao na si la Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) huku wananchi wakihimizwa kuzitunza barabara zinazojengwa katika maeneo yao.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais- TAMISEMI anayeshughulikia miundombinu Mhandisi Rogatus Mativila wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa barabara na madaraja zilizojengwa kwenye kata ya Kibakwe wilayani Mpwapwa.
Mhandisi Matavila alisema kwamba Halmashauri zielewe kwamba suala la kusafisha barabara zilizojengwa kwenye Halmashauri, Miji na Majiji yao ni jambo la kwao na hivyo wanatakiwa kuhamasishana waweze kusafisha.

“Tumeshaletewa barabara nzuri tuzitunze ili zitusaidie sisi wenyewe, mwananchi una nyumba hapo pembeni ya barabara ni vyema kujitoa kusafisha hizo nyasi kandokando ya barabara,”alisisitiza.

Kwa upande wa ujenzi wa barabara zinazotekelezwa na TARURA wilayani Mpwapwa alisema Mji umeanza kupendeza kwani tayari ujenzi wa barabara, madaraja pamoja na uwekaji wa taa unaendelea.
Katika Kata ya Kibakwe TARURA imeshajenga barabara ya lami yenye urefu wa Km. 1.8 na barabara ya Km. 1 iko kwenye hatua za ujenzi ambapo lengo ni kufikia Km. 2.8 Za ujenzi wa barabara katika mji huo ifikapo mwezi Septemba mwaka huu.

“Tunaishukuru Serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutafuta fedha za ujenzi wa barabara nchini.

“Serikali imeona umuhimu wa maendeleo ya barabara za mijini pamoja na kuondoa vikwazo kwa sababu yakukosekana kwa vivuko au madaraja, Mhe. Rais ametafuta fedha kwa lengo la kuhakikisha Makao Makuu ya Wilaya zote pamoja na Miji mikubwa inayokuwa angalau ziwe na lami ili kuunganisha barabara za mijini ambapo sehemu nyingi sana tayari zimejengwa barabara za lami,”aliongeza.
Naye, Afisa Mtendaji wa kata ya Kibakwe Bw. Baraka Zebedayo alisema kupitia Serikali wanafanya uhamasishaji kwa wananchi kuendelea kutunza barabara kwa kufanya usafi kwenye mitaro na pembezoni mwa barabara pamoja na kutokufanya shughuli za kibinadamu kwenye barabara na kila jumamosi ya mwisho wa mwezi wanafanya usafi.

Wakati huo huo Diwani wa kata ya Kibakwe Mhe. Athanas Chisanza alisema wanaishukuru Serikali kwa kuwapatia fedha za ujenzi wa barabara na hivyo kuchochea kasi ya maendeleo katika Kata yao na wananchi kwa ujumla.
Alisema baada ya kuwekewa lami wananchi wao wamepata maendeleo makubwa kiuchumi kwani kata yao ni wazalishaji wakubwa wa mazao hivyo imewarahisishia shughuli za usafirishaji ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo barabara hizo zilikuwa mbaya sana.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news