NA GODFREY NNKO
WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imesema kwamba, ina zaidi ya Hatimiliki 30,000 ambazo zimekamilika, lakini hazijachukuliwa na wamiliki wa ardhi walioomba hatimiliki hizo kutoka katika Masjala za Ardhi katika mikoa mbalimbali nchini.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma leo Julai 30,2024 na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Anthony Sanga.
"Hatimiliki hizi zinajumuisha hatimiliki za kielekitroniki ambazo wamiliki wake wamepewa ujumbe mfupi wa maandishi (sms) kuhusu utayari wa hatimiliki za maeneo hayo katika mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.
Kutokana na hali hiyo, wizara inatoa taarifa kwa wamiliki wote wa ardhi nchini ambao waliomba hatimiliki katika vipindi tofauti na maeneo mbalimbali kwenda kuchukua hatimiliki zao katika Masjala za Ardhi zilizopo katika maeneo vilipo viwanja au mashamba yao wakiwa na kitambulisho cha NIDA.
"Aidha, orodha za hatimiliki zilizokamilika imebandikwa katika mbao za matangazo zilizopo katika Ofisi za Ardhi za mikoa na halmashauri zote nchini.
"Kwa upande mwingine wizara inaelekeza halmashauri zote nchini na Ofisi za Ardhi za mikoa kukamilisha maombi ya hatimiliki yaliyowasilishwa na wananchi au yaliyokwama kwa sababu mbalimbali ndani ya muda wa wiki moja kuanzia tarehe ya taarifa hii,"amesisitiza Katibu Mkuu Mhandisi Sanga.