Haya ndiyo atakayoyafanya Rais Dkt.Samia akiwa Katavi siku nne

KATAVI-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan amewasili mkoani Katavi kwa ziara ya siku nne.
Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amewasili leo Julai 12,2024 ambapo licha ya kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo atazungumza na wananchi.

"Nimewasili mkoani Katavi ikiwa ni siku ya kwanza ya ziara yangu ya kikazi ya siku nne mkoani hapa.

"Nikiwa hapa, nitazungumza na wananchi, nitakagua na kushuhudia hatua kubwa za maendeleo ambazo tumezipiga kwa pamoja, na kushirikishana mipango ijayo.

"Takribani miezi mitatu ijayo tunatarajia kuiunga Katavi kwenye Gridi ya Taifa ili kupata umeme wa uhakika, ikiwa ni matokeo ya kukamilika kwa kazi nzuri ya ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme yenye uwezo wa kilovolti 132 ya urefu wa kilomita 383 kutoka Tabora hadi Mpanda, moja ya njia ndefu zaidi za kusafirisha umeme katika eneo la Afrika Mashariki.

"Pia, nikiwa Katavi nitajumuika na wananchi na kuzindua rasmi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Katavi ambayo sasa ujenzi wake umekamilika, na kuondoa changamoto waliyokuwa nayo wananchi ya kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za afya za kibingwa.

"Asilimia kubwa ya wananchi wa mkoa huu ni wakulima. Ili kuendelea kuinua maisha yao zaidi kupitia kazi yao, tumetekeleza mpango wa kujenga silo ya kuhifadhi nafaka Mpanda, sambamba na Bandari ya Karema kwenye Ziwa Tanganyika kuiunganisha Katavi na masoko ya majirani zetu, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia na Burundi.

"Hatua hizi mbili zinatoa soko la uhakika kwa kilimo na uchumi kwa wananchi wa Katavi na mikoa jirani.

"Katavi inabadilika. Faraja kubwa kuona wananchi wa Katavi wakizitumia fursa hizi mpya kupiga hatua kubwa ambazo sasa zinaonekana, ikiwemo ongezeko la watu kutoka mikoa mingine kufuata fursa Katavi,"amefafanua Mheshimiwa Rais Dkt.Samia.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news