NA GODFREY NNKO
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan leo Julai 31,2024 ameshiriki katika kilele cha Kumbukizi ya Tatu ya Urithi wa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, hayati Benjamin William Mkapa.
Chini ya Wakfu wa Benjamin Mkapa (Benjamin Mkapa Foundation) kumbukizi ya mwaka huu inachagizwa na kaulimbiu ya "Katika Kuchagiza Uendelevu wa Ndani kuelekea Uelekeo Mpya."
BMF ni shirika lisilo la faida lililojitolea kuboresha matokeo ya afya kupitia suluhisho bunifu za afya na mifumo inayohusiana.
Lilianzishwa Aprili 2006 na hayati Rais Benjamin William Mkapa, BMF inafanya kazi Tanzania Bara na Zanzibar, kwa maono ya kuhakikisha maisha yenye afya na ustawi kwa wote nchini Tanzania na Afrika zima
Hafla hiyo imefanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) kilichopo jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia ambaye ni mgeni rasmi amesema kuwa, ni miaka minne tangu atangulie Rais hayati Benjamin William Mkapa mbele za haki.
"Hata hivyo mioyo yetu imeendelea kuwa na kumbukumbu ya urithi na maarifa katika mifumo ya nchi yetu.
"Tunaendelea kuishi nayo hadi sasa, kukutana kwetu hapa siyo kwa sababu tarehe ya kumbukizi imewadia bali yapo mengi ya kukumbuka na sababu nyingi za kukumbuka aliyotuachia mpendwa wetu.
"Katika hali ya kawaida tukio hili la kumbukizi ya mzee wetu lingeweza kuishia kuwa la wanafamilia tu ama tungeweza kuifanya shughuli hii kwa misa kubwa kule kanisani ikaishia huko.
"Lakini tunakutana leo kwa wingi huu na kwa ukubwa huu kwa sababu hayati Rais Mkapa ametuachia sadaka inayoendelea, inayosimamiwa vema na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation.
"Tunakutana leo kuhitimisha mjadala ulioanza siku mbili zilizopita kuhusu suala ambalo hayati mpendwa wetu Benjamin William Mkapa alilipenda na kutuachia kuhusu nguvu kazi katika sekta ya afya."
Pia, amewapongeza wote ambao wapo katika maonesho kando ya kumbukizi hiyo ambapo ameshuhudia bunifu mbalimbali kutoka kwa vijana wa Mkapa Fellowship na mambo mengineyo.
"Kingine kilichonivutia ni kukuta benki inajishirikisha kwenye kutoa mikopo kwa sekta binafsi kuanzisha vituo vya afya.
"Lakini, pia kutoa fedha za kusomesha wahudumu katika sekta ya afya, hilo nalo limenivutia."
Pia, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia amempongeza Msarifu wa Benjamin Mkapa Foundation, Rais Dkt.Hussein Ali Mwinyi, Bodi ya Wadhamini na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo kwa maono mazuri kupitia taasisi hiyo.
Awali, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo, Thobias Makoba amesema,hayati Benjamin William Mkapa anakumbukwa kwa mambo mengi.
"Pamoja na kwamba Benjamin Mkapa Foundation kama taasisi imejikita zaidi katika kutoa huduma na kusaidia sekta ya afya kama eneo lao kuu la kazi.
"Lakini, kumbukizi ya mwaka huu ina mawanda tofauti kwa ridhaa yako Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa mgeni rasmi naomba nitaje japo machache ikiwa ni kuhuisha na kuonesha kazi ya Mheshimiwa hayati Benjamin William Mkapa kwamba hakuwa tu kwenye afya bali kuna mambo mengine.
"Mheshimiwa Rais, la kwanza ni kuhusu Dira ya nchi yetu. Mheshimiwa Benjamin William Mkapa mnamo wakati wa awamu yake ya kwanza alipewa kibali na Mwenyezi Mungu kuandaa dira ya kwanza ya muda mrefu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
"Dira hiyo ilianza kutumika mwaka 2000 na inatupeleka mpaka mwaka 2025. Pamoja na sekta zote kuguswa wewe Mheshimiwa Rais katika sekta hizo ambazo Mheshimiwa Mkapa alizifanyia kazi ndiye Rais wa pili ambaye katika awamu yako ya kwanza uliopokea, umeendeleza na unaenda dira inayofuata ya miaka 25 toka 2025 kwenda 2050.
Hivyo basi tunavyofanya kumbukumbu ya Mheshimiwa Benjamin William Mkapa vile vile na dira inayofuata inabeba maono ya Watanzania kuanzia sasa kwenda mwaka 2050."
Pia amesema, Mheshimiwa amekuwa akitekeleza miradi ya kiuchumi na kimageuzi.
"Kama tunavyofahamu kesho unakwenda kuzindua kwa mara ya kwanza safari za treni ya SGR kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma wapo wanaofahamu, lakini wapo ambao hawafahamu kwamba mradi huu wazo zilianzia Awamu ya Tatu ambayo Mzee Benjamin William Mkapa alikuwa Rais.
"Wewe umebeba mzigo mzito zaidi wa kuhakikisha kwamba siyo tu kilomita 720 zinajengwa lakini umehakikisha tunakwenda mpaka kilomita 2300.
"Hakuna namna bora ya kumkumbuka na kumuenzi Benjamin William Mkapa kama kuendeleza sehemu ya yale aliyoyaona kwa faida kwa Watanzania.Hii inajibu kwa vitendo dhana yako ya Kazi Iendelee."
Pia, amesema kuwa Mheshimiwa Rais Dkt.Samia anamuenzi kwa vitendo hayati Benjamin William Mkapa kwa kuwa muumini wa uhuru wa vyombo vya habari nchini.