DAR-"Pale Benki Kuu ya Tanzania tumejifunza sana jinsi ambavyo unaweza kuwekeza katika Dhamana za Serikali na unajua, watu wengi wanaofanya kazi au wafanyabiashara hawajui kama unaweza kuwekeza pia katika Dhamana za Serikali.
"Kwa hiyo pale tumeona kuna elimu nzuri sana na watu wanaweza kuwekeza kwenye Dhamana za Serikali na wakapata hela bila matatizo. Kwa hiyo, Benki Kuu ukiangalia wanahakikisha kuwa, wanatekeleza zile Sera za Fedha na wakati ninaongea na Gavana inaonesha hata mifumuko ya bei imepungua," ameeleza Naibu Katibu Mkuu Huduma za Hazina Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Christian Omolo, alipotembelea Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere, Barabara ya Kilwa, Temeke, jijini Dar es Salaam na kufanya mahojiano na Hazina TV.