NA DKT.OMARY MOHAMED MAGUO
SHAIRI la hamasa na shamrashamra za kusherehekea miaka 30 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Kilele cha maadhimisho kitakuwa ni tarehe 30 Novemba, 2024 na ikitanguliwa na matukio mbalimbali mpaka kufikia tarehe hiyo.
Karibuni sana wananchi, wahitimu, wanafunzi, na wadau wote wa elimu tusherehekee mafanikio makubwa ya miaka 30 ya OUT.
SHAIRI NAMBARI MBILI
1
Thelathini kutimia, Huria inapendeza
Nguvu kazi Tanzania, Huria imeongeza
Mijini na vijijia, huduma zimechanuza
Heko kwa chuo Huria, Thelathini kutimiza
2
Fursa kimefunguwa, makundi kimefikia
Hakuna kubaguliwa, kwa jina wala jinsia
Wabara na wa visiwa, me'soma chuo Huria
Heko kwa Chuo Huria, Thelathini kutimiza
3
Walobanwa majukumu, ya kazi na familia
Me'soma wakahitimu, bila kazi kuachia
Wakaipata elimu, manufaa Tanzania
Heko kwa chuo Huria, Thelathini kutimiza
4
Kwa umma wanahudumu, mandeleo kupatia
Kwa weledi ukarimu, jamii yafurahia
Kwa ujuzi na ufahamu, wahitimu mardhia
Heko kwa chuo Huria, Thelathini kutimiza
5
Alumni wabunifu, zao chuo Huria
Wamejawa uzoefu, bingwa kujitafutia
Kwenye kazi watiifu, ujuzi wanatumia
Heko kwa chuo Huria, Thelathini kutimiza
6
Chuo chetu twakisifu, nchi nzima kufikia
Kimepunguza urefu, wasoma umetulia
Kwa nafuu masurufu, ada ya chuo Huria
Heko kwa chuo Huria, Thelathini kutimiza
7
Wa Huria tujipambe, kwa furaha tabasamu
Tuwe mbele tujigambe, tutuma zetu salamu
Na Mwenyezi tumuombe, Huria yetu idumu
Heko kwa chuo Huria, Thelathini kutimiza
MTUNZI
Dkt.Mohamed Omary Maguo
Mshairi wa Kisasa
Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Itifaki
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.