TABORA-Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetoa wito kwa wananchi na wapiga kura wa Mkoa wa Tabora kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika kwenye mikoa hiyo kuanzia Julai 20 hadi 26,2024.
Akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Tabora leo Julai 8, 2024, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe.Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele amesema uboreshaji huu unamhusu kila mwananchi mwenye sifa ya kuandikishwa kuwa Mpiga Kura.
“Ni vyema mkatambua kuwa uboreshaji huu unamhusu kila mwananchi mwenye sifa ya kuandikishwa kuwa mpiga kura na anayeboresha taarifa zake. Hivyo, natoa rai kwenu kuwahimiza wananchi kupitia majukwaa yenu ya kisiasa, kijamii, kitamaduni, kiimani na kiuchumi wajitokeze kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura,” alisema Jaji Mwambegele.
“Kila chama kitaruhusiwa kuweka wakala mmoja kwenye kituo cha kuandikisha wapiga kura kwa lengo la kushuhudia utekelezaji wa zoezi la uboreshaji kituoni ikiwemo kuwatambua wale wanaokuja kituoni kama wana sifa za kuandikishwa,” amesema Jaji Mwambegele.
Washiriki wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mkutano huo.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K (kulia) akifafanua jambo wakati wa Mkutano wa wadau wa uchaguzi uliofanyika leo Julai 8, 2024 Mkoani Tabora. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ilikutana na wadau wake Mkoani Tabora kuwataarifu kuhusiana na zoezi la uboreshaji linalotaraji kuanza Julai 20, 2024 mkoani humo.Kulia ni Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele.
Akiwasilisha mada wakati wa mkutano huo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima, R. K, amesema mkoa wa Tabora Tume inatarajia kuandikisha wapiga kura wapya 259,989.
“Hii ikiwa ni ongezeko la asilimia 17.8 ya wapiga kura 1,463,665 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Hivyo, Tume inatarajia baada ya uandikishaji Mkoa wa Tabora utakuwa na wapiga kura 1,723,654,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa lengo la kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, uboreshaji kwa awamu ya kwanza utafanyika kwenye mizunguko 13 itakayobainishwa kwenye ratiba.
“Zoezi hili litaendeshwa kwa siku saba kwenye kila kituo cha kuandikisha wapiga kura. Tunatarajia zoezi litakamilika Machi, 2025,” amesema.