KATAVI-Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi imetoa wito kwa wananchi na wapiga kura wa Mkoa wa Katavi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika kwenye mkoa huo kuanzia tarehe 20 hadi 26 Julai, 2024.
Akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Katavi leo tarehe 08 Julai, 2024, Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Asina Omari amesema kufanikiwa kwa zoezi hilo kunategemea sana ushirikiano wa wadau wa uchagauzi katika kuwahamasisha wananchi.
“Tume inatarajia kupata ushirikiano mkubwa zaidi kutoka kwenu, kwa kuwafikishia wananchi wa mkoa wa Katavi taarifa sahihi na kwa wakati zinazohusu zoezi lililopo mbele yetu la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura na kuwahamasisha wananchi wenye sifa ya kujiandikisha kuwa wapiga kura, wajitokeze kwa wingi kwa tarehe ambazo Tume imeziweka kwa kila kituo,” amesema Mhe. Asina.
Amewapongeza wananchi na wadau wa uchaguzi wa mkoa wa Katavi kwa mkoa wao kupata fursa ya kuwa miongoni mwa mikoa ya mwanzo kufanya zoezi hili la uboreshaji wa Daftari.Akiwasilisha mada kwenye mkutano huo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Bi. Giveness Aswile amesema uzinduzi wa uboreshaji utafanyika mkoani Kigoma Julai 20, 2024 ambapo zoezi litaanza siku hiyo kwenye mkoa huo na mikoa ya Katavi na Tabora.
“Siku ya uzinduzi ndiyo siku ambayo pia uboreshaji utaanza katika Mkoa wa Kigoma sambamba na mkoa huu wa Katavi na Tabora na kufuatiwa na Kagera na Geita,” amesema Bi. Aswile.
Ameongeza kuwa, kwa lengo la kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi, uboreshaji kwa awamu ya kwanza utafanyika kwenye mizunguko 13 itakayobainishwa kwenye ratiba.