Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) yaridhishwa kuendelea kuimarika shughuli za kiuchumi nchini

NA GODFREY NNKO

KAMATI Sera ya Fedha (MPC) ya Bodi ya Wakurugenzi wa Benki Kuu ya Tanzania imesema, imeridhishwa na kuendelea kuimarika kwa shughuli za kiuchumi nchini.

Ni kutokana na utekelezaji wa sera thabiti na maboresho mbalimbali yenye lengo la kukuza uchumi.

Hayo yamesemwa Julai 4,2024 katika ofisi za makao makuu ndogo ya BoT jijini Dar es Salaam na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Sera za Uchumi na Fedha), Dkt. Yamungu Kayandabila kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Sera ya Fedha (MPC) wakati akitangaza Riba ya Benki Kuu kwa robo ya tatu Julai hadi Septemba, 2024.

Katika mkutano huo, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetangaza kuendelea kwa ukomo wa riba ya asilimia 6 katika robo ya tatu ya mwaka 2024 kati yake na benki za biashara nchini.

Riba hiyo itatumika katika kipindi cha robo ya tatu kuanzia Julai 4,2024 hadi Septemba, mwaka huu.

"Hali hii ya kuimarika kwa uchumi inatarajiwa kuendelea katika siku zijazo, kufuatia hali nzuri ya hewa kwa ajili ya shughuli za kilimo, upatikanaji wa uhakika wa umeme, uboreshaji wa miundombinu hususani reli, barabara, na bandari pamoja na sera na programu za maboresho."

Amesema, baadhi ya maeneo mahsusi ya mwenendo wa uchumi yaliyofanyiwa tathmini na kamati hiyo ni pamoja na ukuaji wa uchumi kwa asilimia 5.1 mwaka 2023, ikilinganishwa na ukuaji wa asilimia 4.7 mwaka 2022.

"Ukuaji huu ulichangiwa zaidi na shughuli za kilimo, uchimbaji madini na mawe, ujenzi na shughuli za kifedha hususani ongezeko la mikopo kwa sekta binafsi."

Aidha, amesema shughuli za utalii ambazo zinategemeana na sekta nyingine za uchumi zimeendelea kuchangia kuimarika kwa uchumi nchini.

"Kamati inakadiria ukuaji wa uchumi kuwa takribani asilimia 5 na 5.4, katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2024,mtawalia."

Vilevile, Dkt.Kayandabila amesema,mwenendo wa uchumi wa Zanzibar umeendelea kuwa imara, ambapo ulikua kwa asilimia 7.4 mwaka 2023, ikilinganishwa na asilimia 6.8 mwaka 2022.

"Mwenendo huu unachangiwa kwa kiasi kikubwa na shughuli za utalii, huduma za chakula na uwekezaji kwenye sekta ya ujenzi. Mwenendo huu wa ukuaji wa uchumi nchini unatarajiwa kuendelea katika nusu ya pili ya mwaka 2024 na 2025."

Wakati huo huo Dkt.Kayandabila amesema, mfumuko wa bei uliendekea kuwa tulivu na chini ya kiwango cha asilimia 5 cha vigezo vya utangamano vya kikanda kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).

"Mwezi Aprili na Mei 2024, mfumuko wa bei ulikuwa asilimia 3 na 3.1,mtawalia. Mwenendo huu ulitokanana kupungua kwa mfumuko wa bei wa chakula kufuatia uwepo wa chakula cha kutosha nchini, pamoja na sera thabitiza fedha na bajeti."

Amesema,kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei umeendelea kupungua hadi kufikia takribani asilimia 5, kutokana na kupungua kwa bei za chakula na bidhaa zisizo za chakula.

"Mfumuko wa bei unatarajiwa kubaki ndani ya wigo wa asilimia 3-4, katika nusu ya pili ya mwaka 2024 na kuendelea, ikichagizwa na utekelezaji wa sera thabiti za fedha na bajeti, upatikanaji wa chakula cha kutosha, upatikanaji wa uhakika wa nishati ya umeme, na kushuka kwa bei za bidhaa katika soko la dunia.

"Kuendelea kuimarika kwa hali ya uchumi, kumechangia kwa kiasi kikubwa ukuaji imara wa mikopo kwa sekta binafsi na utulivu wa sekta ya fedha."

Naibu Gavana huyo amesema,katika robo ya pili ya 2024,mikopo ya sekta binafsi inakadiriwa kukua kwa wastani wa asilimia 16.4 ikilinganishwa na asilimia 17.1 katika robo iliyotangulia.

Pia, amesema sekta ya benki iliendelea kuwa na ukwasi na mtaji wa kutosha huku ikitengeneza faida. Aidha, amana, rasilimali na mikopo imeendelea kuongezeka.

"Ubora wa rasilimali za benki umeendelea kuimarika,kufuatia kupungua kwa kiwango cha mikopo chechefu hadi asilimia 4.4 Mei 2024, ndani ya wigo unaokubalika wa chini ya asilimia 5,na asilimia 5.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.

"Mikopo kwa sekta binafsi inatarajiwa kuendelea kuongezeka katika kipindi kijacho cha mwaka 2024 kutokana na kuimarika kwa hali ya uchumi wa dunia na wa ndani."

Mbali na hayo amesema,utekelezaji wa bajeti ya Serikali umeendelea kuwa wa kuridhisha huku ukichagiza utekelezaji wa sera ya fedha.

Kwa upande wa mapato ya ndani kwa Tanzania Bara,Dkt.Kayandabila amesema yanakadiriwa kufikia asilimia 95 ya lengo.

Aidha, kwa upande wa Zanzibar,mapato yanakadiriwa kuvuka lengo kwa asilimia 0.3 kutokana na maboresho katika usimamizi wa kodi na kuongezeka kwa utayari wa wananchi kulipa kodi.

Naibu Gavana amesema,katika mwaka 2024/25, Serikali inakusudia kutekeleza sera inayolenga kupunguza matumizi na kuendelea kutekeleza programu ya Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) ya Extended Credit Facility (ECF), pamoja na programu ya Resilience and Sustainability Facility (RSF).

"Urari wa malipo ya kawaida uliendelea kuimarika, kuendana na kupungua kwa athari za mitikisiko ya kiuchumi duniani.

"Mauzo nje ya nchi yaliongezeka kutokana na uuzaji wa dhahabu,mazao asilia na shughuli za utalii.

"Uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje uliongezeka japo kwa kiwango kidogo ikilinganishwa na mauzo ya nje.

"Hivyo, nakisi ya urari wa malipo ya kawaida (current account deficit) inakadiriwa kupungua hadi dola milioni 959.2 katika robo inayoishia Juni 2024 ikilinganishwa na dola milioni 977.8 katika kipindi kama hicho mwaka 2023."

Dkt.Kayandabila amesema,kwa upande wa Zanzibar, urari wa malipo ya kawaida unakadiriwa kuwa ziada ya dola za Marekani milioni 421.5 katika mwaka unaoishia Juni 2024, ikilinganishwa na ziada ya dola milioni 411.5 katika kipindi sawia cha mwaka 2023.

Amesema,hali hii ilitokana na kuongezeka kwa mapato yatokanayo na huduma, hususani utalii.

"Nakisi ya urari wa malipo ya kawaida inatarajiwa kuendelea kupungua hadi asilimia 3.2 ya Pato la Taifa katika kipindi kilichobaki cha mwaka 2024,"amefafanua Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (Sera za Uchumi na Fedha), Dkt. Yamungu Kayandabila kwa niaba ya Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Emmanuel Tutuba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news