DAR-Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga amewataka Wataalam katika Wizara ya Nishati na taasisi zake kujikita katika kufanya kazi kwa kasi, umakini na bidii ili kuwafikishia wananchi nishati ya uhakika na kwamba hicho ndicho kiwe kipimo kikuu cha kutangaza kazi za wizara kwa wananchi.
Kamishna Luoga amesema hayo wakati alipotembea Banda la Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara (SABASABA) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.


Ameeleza kuwa, Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuhakikisha kuwa inatoa fedha za kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji umeme pamoja na miradi mingine ya Nishati akitolea mfano mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) unaotekelezwa kwa kiasi cha shilingi trilioni 6.5 ambao sasa umefikia asilimia 98.
Ametaja baadhi ya miradi mingine ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa kuwa ni pamoja na ya usafirishaji umeme itakayounganisha Mkoa wa Katavi na Kigoma kwenye gridi ya Taifa ambayo ni mradi wa usafirishaji umeme kutoka Tabora hadi Katavi na Tabora hadi Kigoma pamoja na miradi ya kuboresha upatikanaji umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.



Aidha, amewataka wadau wa nishati hiyo kuhakikisha kuwa wanakuwa na kanzidata itakayojumuisha masuala mbalimbali ikiwemo idadi ya wananchi wanaotumia nishati iliyosafi, matumizi yake n.k ambayo itatumika kama moja ya njia za kujitathmini katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia na kuchukua hatua stahiki zitakazowezesha mkakati huo kutekelezwa kwa ufanisi.