Kampeni ya Kilimo ni Mbolea kuchochea matumizi sahihi ya mbolea,usajili wa wakulima

RUVUMA-Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imesema, matumizi sahihi ya mbolea katika uzalishaji wa mazao ni muhimu kwa lengo la kurutubisha na kuboresha afya ya udongo ili kuweza kuzalisha mazao kwa wingi kati eneo dogo.
Kauli hiyo imetolewa wilayani Mbinga na Mkurugenzi mtendaji wa Mamlaka hiyo, Joel Laurent alipozungumza na kusanyiko la wakulima wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya TFRA ijulikanayo kwa jina la KILIMO NI MBOLEA.

Ni kampeni yenye lengo la kuhimiza matumizi sahihi ya mbolea na kuhamasisha wakulima kujisajili na kuuhisha taarifa zao kwenye mfumo wa mbolea ya ruzuku, ili waendelee kunufaika na mpango huo.

Mkurugenzi huyo amesema, idadi ya watu inaongezeka kila kukicha hivyo matumizi sahihi ya mbolea shambani ni muhimu ili kuongeza tija na kutosheleza mahitaji ya chakula kukidhi idadi ya watu iliyopo.

Aidha,Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa ukuaji wa miji, miundombinu na huduma nyingine za kijamii unapunguza eneo linalofaa kwa kilimo na hivyo eneo linalobaki linatakiwa kutumika kwa ufanisi kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea kwa kuongeza tija.

Sambamba na hilo Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa, kuongeza tija ya uzalishaji kupitia matumizi sahihi ya mbolea kunachangia kuongeza kipato cha mkulima mmoja mmoja, ukuaji wa Sekta ya Kilimo na pato la taifa kwa ujumla, hivyo ni matarajio ya TFRA kuwa kupitia kampeni ya KILIMO NI MBOLEA wakulima watanufaika katika shughuli zao za kilimo kwa ujumla.
‘‘Kampeni hii ni muhimu kwa wakulima wote wakati huu tukielekea kwenye msimu wa kilimo wa mwaka 2024/2025, matarajio yetu ni kwamba hamasa ya usajili wa wakulima kwenye mfumo wa mbolea ya ruzuku itaongezeka na hivyo wakulima kunufaika na mpango wa mbolea ya ruzuku na kuongeza tija baada ya kuitumia mbolea hiyo kwa usahih,’’ alisema Mkurugenzi huyo.

Akielezea hali ya matumizi ya mbolea nchini Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa matumizi yameongezeka kutoka tani 363,599 katika msimu wa 2021/22 hadi kufikia tani 840,714 katika msimu 2023/24. Huku akiutaja mkoa wa ruvuma kuwa ni moja ya Mikoa ya Kimkakati ya uzalishaji wa chakula nchini kwa miaka ya hivi karibuni na unaongoza kwa matumizi ya mbolea.
‘‘Katika msimu wa kilimo wa mwaka 2022/23 Mkoa wa Ruvuma ulitumia kiasi cha tani 83,472 ukifuatiwa na Mikoa ya Njombe tani 75,358, Mbeya tani 75,252, Songwe tani 71,230 na Mkoa wa Iringa tani 44,214 hii ni mikoa yenye matumizi makubwa ya mbolea nchini. Kwa mwaka 2023/24 Mkoa wa Ruvuma umetumia tani 113,000 za mbolea na kufanya Mkoa huu kuwa ni miongoni mwa Mikoa tegemezi katika uzalishaji wa chakula’’, alibainisha Mkurugenzi huyo.

Nae Mkurugenzi wa uzalishaji wa ndani na uagizaji wa mbolea kwa pamoja wa mamlaka hiyo Louis Kasera, amesema ili wakulima waweze kunufaika na Mbolea ni vema waende kujisajili kwenye mfumo wa mbolea ya ruzuku na wakulima waliojiandikisha waende kuuhisha taarifa zao.

Kwaupande wake balozi wa kampeni ya KILIMO NI MBOLEA Abdallah Nzunda maarufu Mkojani aliwasisitizia wakulima kutoa ushirikiano wakati wa kampeni na baada ya kampeni ili waendelee kunufaika na elimu inayotolewa ikiwemo matumizi sahihi ya mbolea na usajili wa wakulima kwenye mfumo wa mbolea ya ruzuku.Kampeni hiyo imezinduliwa na Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga Wilayani Mbinga, na kuhudhuriwa na wakulima zaidi ya 1500 kutoka maeneo mbalimbali ya Mbinga, viongozi wa Sekretarieti za Mkoa wa Ruvuma na Wilaya ya Mbinga, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa dini, na baadhi ya wawakilishi wa makampuni ya Mbolea, ambapo kabla ya uzinduzi wa kampeni hiyo wakulima walipata elimu ya matumizi sahihi ya mbolea na matumizi ya chokaa kilimo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news