Maafisa Masuuli watakiwa kusimamia mali za Serikali kikamilifu

ARUSHA-Serikali imewasisitiza Maafisa Masuuli nchini kuzingatia misingi ya uwajibikaji, ufanisi na uwazi katika kuhakikisha kwamba, mali za umma zinatumika kwa manufaa ya wananchi wote. Rai hiyo imetolewa jijini Arusha na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya usimamizi wa Mali za Serikali wa Wizara ya Fedha, Bw. Ismael Ogaga, wakati akifungua Mafunzo ya Usimamizi wa Mali za Umma kwa Maafisa Masuuli, kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Bi. Jenifa Omolo.
Bw. Ogaga alisema kuwa Maafisa Masuuli wanabeba jukumu kubwa la kuhakikisha kuwa mali za umma zinatumika kwa matumizi yaliyopangwa na kwa manufaa yaliyokusudiwa hivyo mafunzo hayo yatawajengea uwezo ili kupunguza hoja za ukaguzi zinazotolewa na Taasisi za umma mbalimbali ikiwemo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
‘‘Nawaasa kila mmoja wetu akahakikishe kuwa mali za umma zinatunzwa na kufanyiwa matengenezo stahiki na kwa wakati, taarifa zake zinatunzwa katika daftari la mali za Serikali, na zinapoondoshwa ziondoshwe kwa kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo,’’ alisisitiza Bw. Ogaga.

Alisema Serikali imetumia fedha nyingi kuwekeza katika miradi ikiwemo ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere-JNHPP (takribani sh. trilioni 6), ujenzi wa Reli ya kisasa-SGR (takribani sh. trilioni 10.6), ununuzi wa ndege, ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi (takribani sh. bilioni 716.3) pamoja na utekelezaji wa miradi ya maji mijini na vijijini (takribani sh. bilioni 457.4).
Alisisitiza kuwa kutokana na uwekezaji mkubwa na wingi wa rasilimali nchini ni muhimu kuwa na mikakati madhubuti ya kuzisimamia mali hizo ili ziweze kutumika kwa matumizi yaliyokusudiwa na kuiwezesha Serikali kupata manufaa ya uwekezaji uliokusudiwa kwa kipindi kirefu.

‘‘Wizara ya Fedha imefanya jitihada mbalimbali katika kuongeza ufanisi wa usimamizi wa mali za umma nchini ikiwemo kusimika na kuwezesha matumizi ya mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mali za Serikali “Government Assets Management Information Systems - (GAMIS) ambao unatumika kutunza na kuchakata taarifa za mali za taasisi zote za umma hapa nchini,’’ alifafanua Bw. Ogaga. Aliongeza kuwa, Wizara imefanya maboresho katika Sheria ya Fedha za Umma sura 348 pamoja na kuandaa Kanuni mahususi za Usimamizi wa Mali za Umma za mwaka 2024 ikiwa ni utekelezaji wa azma ya kuimarisha Mifumo ya Usimamizi wa Mali za Umma nchini.

Alisema kuwa pamoja na jitihada hizo bado kumekuwa na upungufu katika usimamizi wa mali katika Taasisi za Umma ikiwemo mlundikano wa mali chakavu, utunzaji usioridhisha wa mali, upotevu wa mali za umma, usimamizi usioridhisha wa mali za miradi na zilizotaifishwa pamoja na usimamizi usioridhisha wa mali ghalani.
Alisisitiza Maafisa Masuuli kuwa na mifumo thabiti ya uwajibikaji na kuwa mfano bora kwa wengine katika kuonyesha kwamba mali za umma ni amana ambayo wamekabidhiwa kwa niaba ya Watanzania wote.

Kwa upande wao mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo ambaye ni Mkuu wa Kitengo cha Ununuzi na Ugavi Halmashauri ya wilaya ya Arusha Bi. Hilda Mwangalima, aliishukuru Wizara kwa mafunzo hayo na kuiomba iandae mafunzo kama hayo mara kwa mara hasa namna ya matumizi ya mfumo wa GAMIS ili kuboresha utendaji kazi na kuimarisha usimamizi wa mali za umma.

Mafunzo hayo ya siku moja yalitoa fursa kwa washiriki kupata uelewa kuhusu ufutaji na uondoshaji wa mali za umma ambazo ni chakavu, sinzia, ziada na zilizokwisha muda wa matumizi, usimamizi wa ajali na potevu za mali za umma na mwongozo wa kushughulikia madai ya fidia pamoja na usimamizi wa Mfumo wa Kielektroniki wa Usimamizi wa Mali (GAMIS) pamoja na kuwajengea uwezo washiriki kuhusu sheria, kanuni na miongozi inayohusu masuala ya usimizi wa mali za Serikali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news