KIGOMA-Makamu wa Rais, Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango ameipongeza Wizara ya Nishati kwa usimamizi madhubuti wa miradi mbalimbali ya Sekta ya Nishati hususan miradi ya umeme ambayo inapelekea nchi kuzidi kujiimarisha kiuchumi.


‘’Nimpongeze Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko kwa kuisimamia vyema sekta hii, na pia niwapongeze sana TANESCO kwa kazi nzuri mnayofanya ila ni muhimu sasa mkahakikisha Mkoa wa Kigoma unaingia kwenye Gridi ya Taifa ili kuufungua mkoa huu kiuchumi."
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amemshukuru Makamu wa Rais, kupitia Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za kutosha kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali hususan mradi wa ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Nguruka na kuahidi kuendelea kusimamia miradi ya nishati ili kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika kwa wananchi.
"Nikuhakikishie Mhe Makamu wa Rais sisi Wizara ya Nishati tunakuhakikishia kuwa hatutakuwa kikwazo kwa wananchi kupata umeme bali tunaahidi kuwapatia umeme wa uhakika watanzania wote."
Ameongeza kuwa,wizara itaendelea kutekeleza miradi ya umeme ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa mradi wa umeme wa Igamba Kidahwe hadi Malagarasi ambapo mpaka sasa mkandarasi ameshakabidhiwa eneo la mradi.

Ujenzi huo ukikamilika utaunganisha Wilaya nne za Mkoa wa Kigoma ambazo ni Kigoma Mjini, Buhigwe, Uvinza na Kasulu na pia kuongeza hali ya upatikanaji wa umeme kwa mkoa wa Kigoma kupitia Gridi ya Taifa.