Makusanyo madini yavunja rekodi, Waziri Mavunde atoa msimamo

DODOMA-Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde ameweka wazi makusanyo ya maduhuli kwa Mwaka wa Fedha 2023/2024 ambayo ni Shilingi Bilioni 753 huku akipiga marufuku kwa wageni kuingia kwenye leseni za wachimbaji wadogo.
Mavunde pia ametangaza operesheni maalum kwa watumishi wasio waadilifu na kumtaka Katibu Mkuu wa Wazira ya Madini Mhandisi Yahya Samamba kuwachukulia hatua za haraka atakapowasilisha majina ya watumishi hao.
Akizungumza leo Julai 28, 2024 mjini Dodoma, Mhe. Mavunde amesema katika kipindi cha Mwaka 2023/2024, Wizara ya Madini kupitia Tume ya Madini ilipanga kukusanya jumla ya Sh Bilioni 882.121 kutokana na vyanzo vilivyoainishwa katika Sheria ya Madini Sura ya 123.

Amevitaja vyanzo hivyo ni pamoja na Mrabaha, Ada ya Mwaka ya Leseni, Ada ya Ukaguzi wa Madini, Ada za Kijiolojia, Tozo ya Huduma ya Maabara na malipo ya adhabu mbalimbali.

Amesema, katika kipindi cha kuanzia Mwezi Julai, 2023 hadi Juni 30, 2024, Tume ya Madini ilikusanya jumla ya Shilingi Bilioni 753.815 sawa na asilimia 85.45 ya lengo la makusanyo lililopangwa.
“Makusanyo haya ni sawa na ongezeko la kiasi cha Shilingi Bilioni 76.080 ukilinganisha na fedha zilizokusanywa katika Mwaka wa Fedha 2022/2023 ambapo makusanyo yalikuwa ni Shilingi Bilioni 677.734 kwa lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 822.018,” amesema Mhe. Mavunde.

Mhe. Mavunde amesema kuanzia Mwaka wa Fedha 2019/2020 hadi 2023/2024, makusanyo yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka na kutupa imani ya kufikia malengo ya kukusanya Shilingi Bilioni 999.998 kwa mwaka wa fedha 2024/2025.

“Hapo nyuma kidogo, Wizara ilikuwa ikikusanya kiasi kidogo cha maduhuli ukilinganisha na sasa, mathalan, Mwaka wa Fedha 2014/2015, Wizara ilikuwa na lengo la kukusanya Shilingi Bilioni 209.957 na kufanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 168.043.”

Aidha, amesema Mwaka wa Fedha 2015/2016 lengo la makusanyo lilikuwa ni Shilingi Bilioni 211.957 na kufanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 207.917.

“Hata hivyo, ndani ya kipindi kifupi tunashuhudia ongezeko la makusanyo ya maduhuli yatokanayo na shughuli za uchimbaji wa madini, mabadiliko haya ni mafanikio makubwa ambayo wadau wote wa sekta hii wanatakiwa kujivunia,”amesema Mhe Mavunde.
Wakati huo huo, Mhe Mavunde ametangaza Operesheni maalum kwa wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo wa madini kuingia makubaliano yasiyo rasmi na wageni kutoka nje ya nchi na kuwaruhusu kufanya kazi katika leseni zao.

Amesema, leseni za uchimbaji mdogo wa madini zinatolewa kwa watanzania pekee kwa mujibu wa Kifungu cha 8(2) cha Sheria ya Madini, Sura 123.

Kifungu cha 8(3) cha Sheria ya Madini, Sura 123 kimeweka wazi kwamba, kwa mmiliki wa leseni ndogo ya uchimbaji wa madini, pale atakapohitaji msaada wa kiufundi ambao haupatikani nchini, anaruhusiwa kuingia makubaliano na mgeni kutoka nje ya nchi kupata huduma hiyo baada ya makubaliano hayo kupitishwa na Tume ya Madini.
Hata hivyo amesema, athari kubwa zinazotokana na kutozingatiwa kwa kifungu cha 8(3) ni pamoja na; wachimbaji wengi wadogo waliokuwa wakiendelea na shughuli zao za uchimbaji katika leseni husika huathirika kwa kukosa ajira, kupoteza mitaji yao waliyowekeza wakati wa uchimbaji pia huleta chuki kwa Serikali yao.

“Ni marufuku kwa wamiliki wa leseni kuingiza wageni bila kuwa na mikataba na kibali kwa mujibu wa sheria, hatua kali zitachukuliwa, tutafanya operesheni maalum RMO’s (Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa) kama jambo hili linatokea mkoa wako mpaka Waziri au Naibu Waziri afike, nawe ukusanye virago vyako.,” amesisitiza Waziri Mavunde.

Pia, Mhe. Mavunde amekemea vitendo vya udanganyifu kwenye biashara ya madini pamoja na utoroshaji wa madini vinavyofanywa na watu wachache ambao katika vitendo vyao, wanarudisha nyuma malengo ya serikali.
“Wizara itaendelea kuchukua hatua kali kwa wahusika wote watakaobainika wanajihusisha na utoroshaji wa madini,”amesema Mhe. Mavunde na kumuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba kuchukua hatua za haraka kwa watumishi wa Madini wasio waadilifu.

“Kuna watumishi ngazi ya Mkoa sio waadilifu, wanasaidia upotevu wa mapato Katibu Mkuu nitakuletea majina, uchukue hatua mara moja hatuwezi kuwavumilia,”amesema.

Aidha, amewaagiza Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa (RMO’s) kila mmoja kukusanya maduhuli ipasavyo kulingana na lengo alilopangiwa ili kufikia makusanyo ya Shilingi Trilioni 1 kwa mwaka huu wa fedha 2024/2025.
Katika hatua nyingine Mhe. Mavunde amesema jumla ya leseni na maombi ya leseni 2,648 zimefutwa na kwamba muda sio mrefu maeneo yaliyo wazi yatatangazwa ili wawekezaji wa ndani na nje waweze kuomba maeneo ya kuwekeza na kuyaendeleza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news