Mapambano dhidi ya rushwa, uhalifu ni vipaumbele vya Serikali-Rais Dkt.Mwinyi

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, masuala ya kupambana na rushwa na uhujumu uchumi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali zote mbili katika kuendeleza na kuimarisha utawala bora nchini.
Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ameyasema hayo Julai 11, 2024 katika Ukumbi wa Kimataifa wa Maonesho ya Biashara Nyamanzi uliopo Mkoa wa Mjini Magharibi jijini Zanzibar.

Ni katika Maadhimisho ya Siku ya Mapambano dhidi ya Rushwa barani Afrika kwa mwaka 2024, ambayo kwa mwaka huu kitaifa yamefanyika Zanzibar.

"Maadhimisho haya yanaendelea kuipa heshima kubwa nchi yetu na kuonesha dhamira tuliyo nayo ya kuondosha vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi Tanzania na Afrika kwa ujumla."

Pia, ameipongeza Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu wa Uchumi Zanzibar (ZAECA) kwa kuendeleza ushirikiano na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) ambao vile vile umefanikisha uratibu wa maadhimisho hayo ambayo yamefanikiwa kama ilivyokusudiwa.

"Tanzania ilisaini mkataba wa kuzuia na kupambana na rushwa barani Afrika tarehe 5 Novemba 2003 na kuridhia tarehe 22 Februari 2005.

"Mkataba huu ulianza kutumika nchini tarehe 5 Agosti 2006 ikiwa ni miongoni mwa nchi 48 kati ya nchi 55 zilizosaini na kuridhia mkataba huu.

Amesema, hapa nchini tumekuwa tukiadhimisha siku hiyo tangu mwaka 2018 kufuatia uamuzi wa Umoja wa Afrika wa Julai, 2017 kuitangaza Siku ya Julai 11 kila mwaka kuwa ni Siku ya Maadhimisho ya Kupiga Vita Rushwa barani Afrika.

"Madhumuni ya hatua hii ni kujipima mafanikio yaliyopatikana, na changamoto tulizopitia ili kuzitatua kwa pamoja na hatimaye kuandaa mipango madhubuti na endelevu katika juhudi za kuzuia na kupambana na rushwa."

Amesema, kauli mbiu ya mwaka huu ni Mifumo Madhubuti ya Ulinzi ya Watoa Taarifa, Nyenzo Muhimu katika Mapambano dhidi ya Rushwa."

"Ujumbe huu unazikumbusha na kuzihimiza nchi wanachama kuonesha umuhimu wa kuwalinda watoa taarifa ambao wapo tayari kufichua uovu unaotarajiwa au unaofanyika.

"Uthubutu huu unaonesha nia ya dhati ya kuchukia rushwa kwa vitendo na uzalendo kwa nchi yao."

Rais Dkt.Mwinyi amesema, ujumbe huo umekuja mahususi ikizingatiwa kuwa rushwa inaathiri mifumo ya kitaasisi na kuzorotesha mipango ya kiuchumi.

Katika hatua nyingine amesema, tayari Tanzania imeanza kutumia Sheria ya Mwaka 2015 sura ya 446 katika kumlinda mtoa taarifa na mashahidi kwa makosa mbalimbali yaliyoshuhudiwa yakitendeka kwa kuwapatia ulinzi wa kisheria ili kuongeza mapambano ya uhalifu nchini.

Amesema,sheria hiyo itasaidia ulinzi, kuwapa motisha na kulipa fidia kwa watoa taarifa pamoja na mashahidi ili kuwaongezea imani na kuimarisha usalama wa maisha yao.

"Tayari Tanzania imeanza kutumia Sheria ya Kumlinda Mtoa Taarifa na Mashaidi Sura ya 446 kwa makosa mbalimbali yaliyoshuhudiwa yakitendeka kwa kuwapatia ulinzi wa kisheria watoa taarifa ili kuongeza mapambano dhidi ya uhalifu hapa nchini."

Amesema, kuwepo kwa sheria hiyo kunaisaidia Serikali katika mapambano dhidi ya uhalifu na kujenga jamii na Taifa linalopinga uhalifu.

Sambamba na hilo, hatua hii inakuza hari ya wananchi kujisimamia wenyewe katika kuokoa mali za umma.

"Aidha, Sheria ya Kumlinda mtoa taarifa itasaidia ulinzi, kuwatia motisha na kulipa fidia kwa watoa taarifa na mashaidi ili kuwaongezea imani na kuimarisha usalama katika maisha yao."

Amesema, kwa sasa ZAECA inaendelea kutekeleza majukumu yake chini ya Sheria Na.5 ya mwaka 2023, Sheria ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar baada ya kufutwa kwa Sheria Na.1 ya mwaka 2012.

"Kufutwa kwa sheria hii kumetokea baada ya kubaini kuna umuhimu kuifanyia marekebisho ambayo yataenda sambamba na mabadiliko na kasi ya usimamizi na mapambano dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi hapa nchini."

Amesema, ZAECA  na TAKUKURU zinalazimika kutekeleza mikataba mbalimbali inayohusisha masuala ya kupambana na rushwa kama inavyoelekeza ili kufikia malengo ya Kimataifa ikiwemo kupeana misaada ya kisheria.

Sambamba na ushirikiano wa kitaalamu katika kusaidia kuongeza ufanisi wa kuchunguza pamoja na kurudisha mali zinazopatikana kwa njia za rushwa.

"Kwa hakika, utaratibu huu unapaswa kuendelezwa na kubuni mbinu mbalimbali za uelimishaji ili kusaidia kujenga jamii isiyovumilia vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi." 

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi amefurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na ZAECA na TAKUKURU kwa kipindi cha Julai mwaka 2022 hadi Mei 2024 ambapo ZAECA imefanikiwa kudhibiti na kuokoa fedha jumla ya shilingi bilioni 7.9.

Fedha ambazo zimepatikana kupitia njia mbalimbali zikiwemo kukwepa kulipa kodi, ubadhirifu wa mali, mapato na matumizi mabaya ya ofisi.

Vile vile, ZAECA imeweza kuchunguza na kukamilisha majalada 86 na kuyawasilisha kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kwa kushirikiana na Ofisi ya DPP wameweza kupeleka majalada 29 mahakamani.

Kwa upande wa TAKUKURU wameweza kufuatilia miradi ya maendeleo ya umma yenye thamani ya shilingi trilioni 7 na kukamilisha majalada 900 ambapo majalada 600 yalifunguliwa mahakamani.

"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tunahakikisha kuwa mikataba mbalimbali ya Kimataifa tunayoingia hususani hii ya kupambana na rushwa inafikia malengo yake kwa kasi ya maendeleo tunayoikusudia, kwa kuwa mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi wa mali za umma ndio kipaumbele cha Serikali zetu." 

Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi ametaka jitihada hizo ziendelee, kwani kuzuia rushwa ni jambo la kila mmoja kwa nafasi yake kwa kufuata miongozo ya mikataba ya kuzuia na kupambana na rushwa ili kuijenga jamii ambayo inasimamiwa na misingi ya utawala bora.  

ZAECA 

Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA), Ali Abdallah Ali amesema, Serikali kupita taasisi zake zinazoratibu mapambano dhidi ya rushwa zinaungana na mataifa mengine barani Afrika katika kuadhimisha siku hii ili kutimiza azma ya utekelezaji wa mkataba wa Umoja wa Afrika wa kuzuia na kupambana na rushwa.

Amesema, mkataba huo umeletwa kwa lengo la kufanya tathmini ya maendeleo ya mapambano dhidi ya rushwa Afrika kwa kushirikiana na wadau mbalimbali na kuandaa mikakati itakayotoa ufanisi zaidi katika kukabiliana na rushwa Afrika.

Amefafanua kuwa mashirika hayo ZAECA na TAKUKURU katika kutekeleza mapambana dhidi ya rushwa na uhujumu uchumi yanaendelezwa nchini na yamekuwa na mafanikio katika kubadilisha uzoefu wa kiutendaji baina ya taasisi hizo ili kuhakikisha matokeo chanya ya kusimamia majukumu kwa pamoja.

Awali, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amempongeza Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi kwa kazi nzuri ambayo anaifanya Zanzibar.

"Kwa hakika sisi ambao tunakuja Zanzibar mara kwa mara tunayaona mabadiliko. Yule ambaye amesema yeye hataki, basi yeye mwenyewe ameamua kukataa, lakini kwa kweli kazi nzuri unaifanya na Mwenyezi Mungu akuzidishie sana."

Katika hatua nyingine amempongeza Mheshimiwa Waziri, uongozi wa ZAECA na TAKUKURU kwa kazi nzuri ambayo wanaifanya.

"Na sisi tukuahidi Mheshimiwa Rais kwamba tutaendelea kufanya kazi kadri ambavyo wewe unatutaka sisi tufanye, na hatutachoka, tutaendelea kuwasimamia wenzetu ili malengo yako mazuri ya kuifanya Zanzibar yenye neema ipate kuonekana yanafikiwa,"amesema Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete.Bofya hapa kwa video》》》

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news