NA GODFREY NNKO
WAKIWA wanaongozwa na kauli mbiu ya "Mikakati ya Mashirika na Taasisi za Umma kuwekeza Nje ya Tanzania", viongozi wa taasisi na mashirika ya umma wanatarajiwa kukutana katika mkutano wa pili ambao utafanyika hivi karibuni nchini.
Hayo yamebainishwa leo Julai 15,2024 jijini Dar es Salaam na Msajili wa Hazina,Nehemiah Mchechu wakati akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuhusu kikao chao cha CEOs Forum cha pili.
Kikao cha kwanza kati ya viongozi wa taasisi na mashirika ya umma kilifanyika jijini Arusha kuanzia Agosti 19 hadi 21, 2023 katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC).
"Na kundi hili (viongozi) huwa ninasema ni kundi muhimu sana na ni kikao muhimu sana kwa kweli, kwa sababu katika kile kikao huwa tunakuwa na wenyeviti na ma-CEOs zaidi ya 600.
"Tunapoingia kwenye kada ya wenyeviti mle ndani tuna makatibu wakuu, tuna wakuu wa Majeshi, tuna makatibu wakuu viongozi waliopita kwa hiyo ni kundi ambalo huwa ninasema ni think tanks kubwa inayokuwa under one roof.
"Nilisema mwaka jana changamoto yangu ambayo ninaiona na changamoto sote tuliyonayo ni kwamba unatumiaje lile kundi effective kwa maana ya uzoefu na ubobezi ambao upo ndani ya kundi lile.
"Hii ni changamoto ambayo Mheshimiwa Rais alitupatia alipokuwa ameshiriki na sisi mwaka jana alipokuja kutufungulia ule mkutano wetu wa kwanza.
"Lakini, tunafikiri ni muhimu sana kwa mashirika yetu kuanza kujiuliza wanaweza vipi au tunaweza vipi kuanza kuzitizama biashara zetu nje ya mipaka ya Tanzania.
"Na kuitazama biashara nje ya mipaka ya Tanzania kuna namna nyingi, kuna namna ya kufanya uwekezaji katika hizo nchi, lakini una namna ambayo huduma yako inaenda kuzigusa hizo nchi.
"Tunapozungumza shirika kama la ndege (ATCL) ni kwamba huduma zake zinaenda kugusa nje ya nchi. Unapozungumza shirika kama TRC tunategemea kwamba kwa uwekezaji ule na ili tupate faida na mtaji uweze kurudi kwenda kwenye sehemu zingine basi shirika lile lazima litazame shughuli zake nje ya nchi.
"Lakini, zaidi tumekuwa na mikakati ya kisekta, kuna sekta ambazo tunatamani zikimbie ziende nje ya nchi moja kwa moja kwa mfano tumekuwa na focus kubwa sasa hivi kwenye mabenki.
"Ukiangalia kabisa unaona sasa hivi kuna mabenki mengi ya Kenya yako hapa Tanzania, unaona kabisa kwamba kuna makampuni ya Kenya yapo hapa Tanzania.
"Lakini, unajua siku zote benki ni kama pipeline ambayo inavuta wawekezaji wako wote. Unaweza ukashangaa tuna benki moja tu kwa mfano City Bank wamekuwa na tawi moja tu Tanzania.
"Miaka yote wanatengeneza faida, lakini unajiuliza lengo lao lilikuwa ni nini. Lakini,ukiitazama kwa kina malengo yao ni kusapoti cashflow na biashara za mashirika ya Kimarekani, Tanzania au katika nchi zingine ambako wamefanya uwekezaji.
"Kwa hiyo, nimesema kwa mfano sekta ya kibenki yote ndiyo tumeitazama kwa kina. Tunatamani sana tuone baadhi ya benki zenye mitandao mipana Tanzania zikiwa zinajikita pia nje ya nchi.
"Sasa sisi tuna interest kwenye baadhi ya benki, tuna interest kwenye benki kama NMB, NBC. Tuna interest indirect CRDB, tuna interest TCB sasa hizi benki, nimezitaja hizo lakini kuna benki zingine. Lakini nimezitaja hizi kwa sababu zina mtandao mpana ndani ya nchi," amefafanua kwa kina Mchechu.
Katika hatua nyingine, Msajili wa Hazina ameyataja maeneo muhimu yatakayofanyiwa kazi katika kikao kazi hicho cha pili jijini Arusha kuwa ni kujadili hatua zilizofikiwa katika utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika kikao kazi cha kwanza.
Pia,kujadili na kupata uzoefu wa kiutendaji kutoka kwa wataalam wa ndani na nje ya nchi waliofanikiwa kiutendaji wakiangazia nchi za Singapore, China, Umoja wa Falme za Kiarabu na Afrika Kusini.
Jambo lingine ni namna bora ya kuboresha mitaji ya mashirika ya umma ili kuleta ufanisi wa kiutendaji na kuongeza ushindani.
Aidha,kubadilisha mitazamo na kuzifanya taasisi na mashirika ya umma kuwa vichocheo vya maendeleo ya kiuchumi.
"Na tutapitia kwa pamoja na kukumbushana kuhusu mambo mengine muhimu ambayo wenyeviti wa bodi na watendaji wakuu wanapaswa kuzingatia katika usimamizi wa utendaji kazi ikiwemo miongozo mbalimbali ya uendeshaji wa mashirika ya umma pamoja na umuhimu wake katika kutekeleza malengo ya Serikali kwa ufanisi,"amesema Mchechu.
Vile vile amesema, watajadili changamoto mbalimbali za kiuendeshaji katika taasisi pamoja na kuainisha mikakati ya kukabiliana nazo.
Mchechu amesema, matarajio ni kuona taasisi zinawekeza kwa faida ikiwemo kuongeza ufanisi ambao utawezesha matokeo bora.
"Na taasisi zile zinazofanya biashara zitaongeza faida na hivyo kutoa gawio kwa mujibu wa sheria.Kwa taasisi ambazo zilianzishwa kwa misingi ya kutoa huduma zitaongeza uwezo wa kujitegemea katika uendeshaji wake na kuendelea kuwepo kwa mfumo endelevu wa kuzitambua taasisi zinazofanya vizuri na kuchukua hatua stahiki kwa taasisi ambazo hazifanyi vizuri."
Mkutano huo wa pili ambao unatarajiwa kufanyika mwezi ujao jijini Arusha mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan.
Msemaji Mkuu wa Serikali
Awali, Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo,Thobias Makoba amesema,maagizo aliyo ni kwamba wahariri wanapokutana au wanahabari naye anapaswa kuwepo kwa kuwa ni sehemu ya familia yake.
"Kwa hiyo nimekuja katika kuendeleza, kujenga tasnia yetu ya habari ili kuiendeleza nchi yetu ya Tanzania, zaidi ya hilo lazima tufanye media sessions na wanahabari kwa sababu kuu mbili.
"Kwanza,wao wenyewe waelewe kilichoagizwa na Mheshimiwa Rais, kwa nini CEOs Forum ifanyike kwa maana wanahabari wakielewa ni rahisi umma kuelewa na mtakuwa mmemsikia Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisisitiza mara kwa mara kwamba mashirika ni ya umma, faida, hasara tutakazozitengeneza tunaubebesha mzigo umma.
"Na haitakiwi kuwa hivyo, kwa hiyo daraja kuu la kufikisha taarifa ni vyombo vya habari ambavyo mimi sasa ndiyo nimepewa jukumu la kuwa mlezi nikasema kwa sababu ukiacha tu kuwa Mwenyekiti, lakini kwa kofia ninayovaa sasa hivi lazima niwepo.
"Lakini, vile vile mashirika haya ya umma ni uwekezaji mkubwa wa Tanzania, lakini mashirika haya ya umma na taasisi zimegusa sekta zote.
"Sasa, Msemaji Mkuu wa Serikali yeye hana sekta, amewekwa huku kwa Wizara ya Habari lakini anazungumzia sekta zote.
"Tuchukulie mfano wa ziara ya Mheshimiwa Rais inayoendelea sasa hivi Katavi, alivyoshuka tu uwanjani Mpanda ameenda kuzindua jengo chini ya TAA (Tanzania Airports Authority) akatoka hapo jana amezindua tena maghala yako chini ya NFRA, hivyo hivyo miradi mingine ambayo imeendelea kuzinduliwa. Mashirika hayo yote yapo chini ya Ofisi ya Msajili wa Hazina.
"Hizo ni sekta tofauti, kwa hiyo kwa tafsiri hiyo hata Ofisi yangu mimi inawajibika kwenye sekta zote. Kwa hiyo kukuza mashirika haya au kuyasaidia yakue ni sehemu ya wajibu wetu na namna bora ya kuyakuza ni kuhakikisha Watanzania wanapata habari sahihi, Watanzania wanayajua na hiyo haiwezekani bila kupitia kwa wahariri bila kupitia kwa wanahabari,"amesisitiza Makoba.