Mbibo aishawishi Stanbic Bank kuifikiria Sekta ya Madini nchini

DODOMA-Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo ameishawishi Benki ya Stanbic kuifikiria Sekta ya Madini nchini na kuona namna inavyoweza kushirikiana nayo kutokana na uwepo wa fursa nyingi za kiuwekezaji na kibiashara ikiwemo mifumo mizuri ambayo inaweka usalama uwekezaji wao.
Aidha, ameitaka benki hiyo kufikiria namna inavyoweza kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kufuatia mabadiliko na kuimarika kwa shirika hilo kiuwezaji ikilinganishwa na hapo awali ambapo Serikali ililiweka katika orodha ya mashirika yaliyopaswa kufutwa.
Mbibo ameyasema hayo leo Julai 2, 2024 jijini Dodoma katika kikao baina ya Wizara, STAMICO na Benki hiyo kilicholenga kuifahamisha kuhusu fursa za uwekezaji zilizopo STAMICO na katika Sekta ya madini ikiwemo kufahamishwa kuhusu maendeleo ya Sekta na uzoefu wa shughuli za madini nchini.

"Uamuzi wa Serikali wa kutaka STAMICO ijitegmee kwa asilimia 100 bila kutegemea ruzuku ya Serikali ni alama ya ukuaji. Katika mwaka huu wa Fedha tuliouanza STAMICO hawatapata fedha kutoka Serikalini na ukweli ni kwamba wanahitaji fedha kutoka kwa wadau kama ninyi kuendesha miradi yao na kujiendesha wenyewe pamoja na kuwasaidia wachimbaji wadogo wa madini nchini,’’ amesisitiza Mbibo.
Pia, Mbibo ameueleza ujumbe huo kuhusu fursa ya kibiashara iliyopo kupitia Sekta ndogo ya uchimbaji mdogo hususan katika biashara na kueleza kwamba ni eneo ambalo linahitaji kuwezeshwa kimitaji na hususan dhahabu kutokana na mahitaji makubwa ya madini hayo duniani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Huduma kwa Wateja kutoka Stanbic Bank Group, Anne Aliker, amesema lengo la ziara ya benki hiyo Wizara ya Madini ni kutaka kujua maeneo ambayo benki hiyo inaweza kushirikiana na Sekta ya Madini nchini, kufahamishwa kuhusu miradi muhimu iliyopo kwenye Sekta ya Madini pamoja na kutaka kujua maeneo ambayo benki hiyo inaweza kuanzisha ushirikiano.
Ameongeza kwamba, kutokana na uzoefu wa benki hiyo katika shughuli za madini katika nchi mbalimbali barani Afrika ikiwemo Afrika Kusini pamoja na ushiriki wa benki hiyo kwenye mkutano mkubwa wa uwekezaji Afrika wa Mining Indaba.

Pia, Anne amesema kuwa Sekta ya Madini ni miongoni mwa sekta inayotazamwa na benki hiyo na zaidi Sekta ya Madini Tanzania na kueleza, ‘’pamoja na uzoefu huo bado tunahitaji kuelewa zaidi kuhusu Tanzania,’’
Awali, akielezea katika kikao hicho kuhusu muundo, miradi na maeneo yenye kuhitaji ushirikiano, Meneja wa Ufuatiliaji na Tathmini wa STAMICO David Semeo amesema kuwa ni pamoja na mradi wa upanuzi wa uchimbaji makaa ya mawe Kiwira, kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe, kuendeleza leseni ya madini ya shaba, kuanzisha mfumo wa wachimbaji wadogo na kuanzisha kituo cha mfano kwa ajili ya wachimbaji wadogo cha madini ya chumvi Lindi.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini Dkt. AbdulRahman Mwanga ameueleza ujumbe huo kuhusu dhamira ya Serikali kufanya utafiti wa kina wa madini na kueleza kwamba ni eneo ambalo linahitaji fedha huku akieleza kuhusu umuhimu wa benki hiyo kusaidia mitaji kwenye miradi mikubwa ya uchimbaji madini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news