Mema zaidi yanakuja Kilimo cha Umwagiliaji, wadau wayajenga mkoani Katavi

KATAVI-Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imefanya Mkutano wa Wadau wa Umwagiliaji kwa Skimu za Mwamkulu na Kabage Mkoani Katavi.Mkutano huo umejumuisha wakulima wa kata ya Mwamkulu, wataalamu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Makao Makuu na Mkoa wa Katavi, Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoka, viongozi wa chama ngazi ya Mkoa na wilaya pamoja na wakuu wa wilaya za mkoa wa Katavi.
Akifungua Mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa katavi, Mwanamvua Mrindoko , amewaasa wakulima na wananchi wa kata ya Mwamkulu kutumia fursa ya ukarabati wa miundo mbinu ya umwagiliaji kushiriki katika kilimo ili kuinua kipato chao na kuepuka migogoro isiyo ya lazima, inayoweza kukwamisha juhudi za serikali kuwaletea maendeleo.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa amesisitiza kuhusu nia ya serikali kuendelea kuinua na kuboresha kilimo cha umwagiliaji nchini,kwa kujenga, kuboresha na kuendeleza Miundo mbinu ya Umwagiliaji kwa lengo la kuboresha kilimo cha Umwagiliaji nchini.
Mndolwa amebainisha kuwa Tume imeshapata dhamana ya kuanza na skimu 2 za Mwamkulu na Kabage, ambapo ujenzi unaendelea vizuri na kwamba Mheshimiwa waziri wa Kilimo anakuja kuweka jiwe la msingi.

Mkurugenzi mndolwa pia amesema kuwa Tume inaendelea na ujenzi wa Ghala kubwa la kuhifadhi mazao ili kuhakikisha kuwa wakulima hawauzi mpunga badala yake waweze kuuza mchele.
Mndolwa pia ameongeza kuwa, pamoja na ujenzi huo wa miundo mbinu, Tume pia imeweza kufanya jambo la kijamii, kwa kufanya ukarabati wa nyumba ya mganga na wauguzi wa kituo cha afya cha Mwamkulu pamoja na ukarabati wa jengo la huduma kwa akina mama ma katika kituo hicho.

Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imewekeza zaidi ya Bilioni 54 katika ukarabati na kuboresha Miundo mbinu ya umwagiliaji katika skimu za Mwamkulu na Kabage ambapo wakulima 2500 watanufaika na kwamba miundo mbinu hiyo itahudumia eneo lenye ukubwa wa hekta 6000 katika kata ya Mwamkulu.
Akifafanua hatua zilizofikiwa katika hatua za ukarabati na ujenzi wa miundo mbinu hiyo katika kata ya Mwamkulu,Raymond Mndolwa amefafanua kuwa serikali ya rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, imefanya ujenzi wa bara bara za mashambani, yenye jumla ya urefu wa km 90 na ujenzi wa mitaro iliyosakafiwa, ya kusafirisha maji mashambani, yenye jumla ya urefu wa kilomita 151.52 ikiwa ni mitaro mikuu, ya kati na midogo, itakayo tumika kufikisha maji mashambani.

Kwa upande wake Mhandisi wa Umwagiliaji Mkoa wa Katavi, Samson Bayi, amesema Mkoa wa una jumla ya skimu 29 na kwamba skimu 15 kati ya hizo zimesajiliwa chini ya Tume ya Taifa ya umwagiliaji na kwamba Tume imeshaanza na utekelezaji katika miradi 3 ambapo wakandarasi wanaendelea na kazi.
Akijibu maswali ya wadau Mndolwa amesema Tume ipo tayari kuendelea kushirikiana na wakulima kutatua changamoto ikiwepo utengenezaji wa mabirika kwaajili ya kunyweshea mifugo.Amebainisha pia kuwa wizara imejipanga kuanza na ununuzi wa pawa tila 800 kwaajili ya kuwasaidia wakulima Mwamkulu na kwamba Tume inakwenda kuongeza ghala la pili jipya katika kata ya Mwamkulu.

Amewahimiza pia wakulima wa kata ya Mwamkulu watunze miundo mbinu inayowekwa na serikali na waendelee kulipa ada ya umwagiliaji ili kuchangia juhudi za serikali iweze kujenga na kuendeleza miundo mbinu mahali pengine.Mndolwa pia amehimiza wakulima na wananchi kuendelea kuheshimu sheria zinazo simamia rasimali za maji hususan sheria inayokataza kilimo ndani ya mita 60 kutoka chanzo cha maji.
Mndolwa pia amewakumbusha wadau wa umwagiliaji kuwa serikali imenunua mitambo mikubwa ya ujenzi na ukarabati wa miundo mbinu na kwamba Tume itatumia mitambo hiyo kuwafikishia huduma hizo wananchi wa kata ya Mwamkulu na maeneo mengine yenye uhitaji huo.
Akizungumza kuhusu msimamo na mpango wa serikali, Mndolwa ameeleza wadau kuwa serikali imejipanga kutumia maji ya ziwa Tanganyika kuwawezesha wananchi wa Katavi kupata maji kwaajili ya umwagiliaji, matumizi ya binadamu pamoja na mifugo; na kwamba serikali haipo tayari kuona wakulima wananyanyasika ndani ya nchi yao.
Mkutano wa wadau wa Kilimo cha Umwagiliaji uliyofanyika katika kata ya Mwamkulu umelenga kuwaleta pamoja wadau mbali mbali wa kilimo cha umwagiliaji Mkoani Katavi, kwa lengo la kuendelea kuwaelimisha wakulima na wadau wa kilimo cha Umwagiliaji, kuhusu sheria, kanuni na taratibu zinazo simamamia shughuli za umwagiliaji nchini na kuwapa wadau fursa ya kuibua kero zao na kupatiwa majibu ya kina kutoka kwa wataalam na uongozi wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news