MBEYA-Mahakama ya Wilaya Mbarali mkoani Mbeya imemhukumu aliyekuwa Mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali,Bw. Joseph Werema Ndimila adhabu ya kulipa faini ya shilingi milioni 1.1 au kwenda jela mwaka mmoja.
Vilevile, ameamriwa kurejesha kiasi cha shilingi milioni 4 alichokifanyia ubadhirifu baada ya kukutwa na hatia katika makosa ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdangaya mwajiri.
Kutumia vibaya madaraka na kosa la kufanya ubadhirifu ambayo ni kinyume na vifungu vya 22, 31 na 28 vya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa [CAP 329 R.E 2022].
Hukumu dhidi ya Bw. Ndimila imetolewa Julai 26, 2024 kutokana na shauri la Uhujumu Uchumi Na. 18/2023 lililokuwa katika Mahakama ya Wilaya Mbarali mbele ya Hakimu Mkazi Aliko Michael Mwandumbya.
Ni shauri ambalo liliendeshwa na Mwendesha Mashtaka kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Bw. Sospeter Tyeah.
Ilielezwa kuwa, mshtakiwa alifikishwa mahakamani kwa mashtaka tajwa hapo juu kwa kuandaa nyaraka za uongo za malipo (pay lists) akionesha kuwa aliwalipa watu mbalimbali kwa kukodi kumbi kwa ajili ya kufanya semina katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kulipa jumla ya shilingi 4,000,000 huku akijua kuwa malipo hayo ni ya uongo na alilenga kumdanganya mwajiri wake na kujipatia kiasi hicho cha fedha.
Aidha,Bw. Ndimila amelipa faini yote ya shilingi 1,100,000 na amerejesha kiasi chote cha shilingi 4,000,000 alichokifanyia ubadhirifu.
Tags
Habari
Mahakamani Leo
PCCB Tanzania
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
TAKUKURU Tanzania