KATAVI-Mbunge wa Jimbo la Kavuu katika Halmashauri ya Mpimbwe Mkoa wa Katavi na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mhe. Geophrey Pinda ametoa zawadi za majiko ya gesi kwa walimu wa shule za sekondari za jimbo lake zilizofanya vizuri katika mitihani ya kidato cha sita na cha nne katika Mkoa wa Katavi.
Walimu waliopatiwa zawadi hizo ni kutoka shule za sekondari za Mizengo Pinda iliyoshika nafasi ya kwanza kimkoa kwa upande wa matokeo ya kidato cha sita, shule ya sekondari Usevya iliyoshika nafasi ya nne kidato cha sita kimkoa pamoja na shule ya sekondari Mbede iliyoshika nafasi ya kwanza kwenye matokeo ya kidato cha nne kimkoa.
Mhe. Pinda amezipongeza shule hizo tatu tarehe 18 Julai 2024 kwa kufanya vizuri katika matokeo ya mitihani ya taifa ambapo amesema njia pekee ya kutoa shukran zake kwa shule hizo ni kutoa zawadi kwa walimu ambao shule zao zimefanya vizuri kimkoa ili kuongeza chachu ya mafanikio.
Katika ziara yake hiyo ya kukabidhi zawadi Mhe. Pinda alipongezwa na uongozi wa shule hizo kwa moyo wake wa kutoa zawadi kwa walimu ambapo ulieleza kuwa zawadi hizo ni ishara kuwa mbunge huyo anatambua mchango wao katika matokeo ya mitihani ya taifa kwa kidato cha sita na nne kimkoa.
Hata hivyo, uongozi wa shule hizo ulimueleza mhe. Mbunge baadhi ya changamoto zinazozikabili kama vile upungufu wa walimu, ukosefu wa miundombinu kama vile madarasa,mabweni pamoja na uzio.
Mhe. Pinda aliahidi kuzishughulikia changamoto hizo huku akitoa wito kwa wazazi wa jimbo hilo la Kavuu kushikamana kuchangia masuala ya elimu ili watoto waweze kupata elimu bora itakayowasaidia kwenye maisha yao ya baadaye huku akisisitiza kuwa urithi pekee kwa watoto ni elimu.
Amesema, shule katika jimbo lake zingefanya vizuri zaidi kama wazazi wangekuwa pamoja na kutolea mfano wa utoaji fedha kwa ajili ya chakula kwa wanafunzi wanapokuwa shuleni.