Mheshimiwa Sagini aipa kongole Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, atoa wito

DODOMA-Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Mhe. Jumanne Sagini ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria katika utatuzi wa changamoto mbalimbali pamoja na kutoa huduma bora za kisheria kwa wananchi na Serikali kwa ujumla.
Mhe. Sagini ameyasema hayo mara baada ya kukutana na Watumishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoani Dodoma leo Julai 2, 2024 ambapo amewataka watumishi hao kuendelea kushirikiana huku kila mmoja akitakiwa kuyajua na kuyatekeleza majukumu yake ipasavyo.
Aidha, Mhe. Naibu Waziri amewataka watumishi hao kuendelea kushikamana na kushirikiana katika maeneo yao ya kazi, na pale kunapobainika kuwepo kwa baadhi ya changamoto baina yao, watafute njia bora za kuzitatua bila kuathiri utendaji wa kazi.

“Lengo letu ni Sekta yetu kuweza kupata mahitaji yatakayoweza kusaidia kufanikisha majukumu muhimu kwa wananchi na Serikali katika ubora na ufanisi mkubwa.” 
Mhe. Naibu Waziri alipongeza juhudi na ubunifu uliofanywa wa kuwa na Kliniki ya elimu ya sheria ambayo imelenga kutatua changamoto hizo za kisheria wanazokabiliana nazo wananchi na hatimaye kupata haki stahiki.
Awali, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Balozi Prof. Kennedy Gastorn akisoma taarifa fupi kwa Mhe. Naibu Waziri alitaja baadhi ya mafanikio yaliyopatikana ni pamoja na jumla ya sheria 300 zimefanyiwa tafsiri kwa lugha ya Kiswahili ,huku sheria hizo zikisubiriwa kutangazwa katika toleo la Urekebu la mwaka 2023.

Akifafanua zaidi, Mhe. Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali ametaja mambo kadhaa ambayo, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imefanikisha kuandaa hadi sasa kuwa ni pamoja na maazimio kumi ya kuridhia mikataba na itifaki mbalimbali yaliyoandaliwa na kuwasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Tumeweza kutoa mafunzo mahsusi kwa waandishi wa Sheria, Majadiliano ya Mikataba, na utoaji wa ushauri kwa mawakili 300 wa Serikali kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali ambao wameweza kushiriki katika Mafunzo hayo.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news