Miaka 30:OUT yajivunia Moodle mfumo wake wa ujifunzaji na ufundishaji kielektroniki

NA DKT.MOHAMED OMARY MAGUO

KATIKA uchambuzi huu wa makala ya kwanza sehemu ya kwanza, leo tunapenda kuelezea mfumo wa Ujifunzaji na Ufundishaji Kieletroniki maarufu Moodle wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania unatoa huduma gani kwa wanafunzi.
Hii ni kufuatia shamrashamra na hamasa ya kusherehekea miaka 30 ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT) mwaka huu wa 2024.

Kimsingi, mfumo huu wa Ujifunzaji na Ufundishaji ni mzuri sana ambapo wanafunzi anapoingia anapata maalumati yaani notisi za masomo yake kwa njia mbalimbali. Njia hizo ni hizi zifutazo:

Mosi: Maalumati kwa njia ya Video

Mwanafunzi anapoingia katika mfumo wa Moodle anakuta tayari mwalimu wa somo ameshaandaa maalumati ya somo husika kwa njia ya video kulingana na mada husika.

Hivyo mwanafunzi anapata fursa ya kusikiliza video hizo kwa wakati wake popote pale alipo huku akiongozwa na Course Outline ambayo nayo inapatikana hapo hapo kwenye Moodle.

Video hizo zinaweza kuwa ni mihadhara mbalimbali kutoka kwa mwalimu wa somo au wataalamu wa mada husika kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Hii inampatia mwanafunzi uwanja mpana wa kujifunza na kuelewa mambo kutoka kwa wataalamu mbalimbali.

Pili: Maalumati kwa njia ya sauti

Njia hii hutumiwa na mwalimu wa somo kupakia maalumati kwa njia ya sauti kwenye Moodle.

Hapa mwanafunzi anaweza kusikiliza mihadhara mbalimbali akiwa mahali popote pale alipo.

Atasikiliza sauti za wahadhiri mbalimbali na ikiwa hajaelewa anaweza kurudia tena na tena mpaka aelewe.

Hii ndiyo faida kubwa ya mfumo wa Ujifunzaji na Ufundishaji Kieletroniki unaopatikana Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Tatu: Maalumati kwa njia ya maandishi

Kupitia njia hii, mhadhiri wa somo husika hupakia maalumati yaliyoandikwa na kuandaliwa na wataalamu mbalimbali wa fani na uga husika.

Hapa huwekwa vitabu, majarida, magazeti, makala, Insha za kitaamu na machapisho na maandiko yote muhimu kulingana na mada husika.

Mwanafunzi anapata fursa ya kujisomea kwa kina popote pale alipo bila bugdha kwa raha mustarehe akiwa anaendelea na majukumu yake.

Nne: Maalumati kwa njia ya Picha na Michoro

Hapa mhadhiri wa somo huandaa picha na michoro ambayo itamwezesha mwanafunzi kujisomea na kuelewa zaidi mada husika.

Picha na michoro humwezesha mwanafunzi kuvuta tafakuri ya kilichopo kwenye picha na kuhusianisha na kile alichokisoma kupitia video, sauti na maandishi na hatimaye kuwa na uelewa mkubwa wa mada husika.

Tano: Maalumati kwa njia ya Pawa Pointi

Hii ni njia ya kuwasilisha maalumati kwa maelezo mafupi mafupi ambayo humwezesha mwanafunzi kupata uelewa wa haraka wa mada au somo husika.

Katika mfumo Moodle wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mwanafunzi anapoingia kwenye somo husika anapata maalumati kwa njia ya pawa pointi.

Kupitia dondoo tano hapo juu unaweza kuona kwamba mwanachuo wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania anapata uwanja mpana sana wa kujisomea kupitia njia hizo za upatikanaji wa maalumati kwenye Moodle.

Mwanafunzi ambaye hapendi maalumati kwa njia fulani anapata maalumati yake kwa njia anayoipenda ambayo ipo hapo hapo kwenye mfumo.

Mwanafunzi yupo huru kuchagua asome maandishi, asikilize sauti, atazame na kusikiliza video, asome pawa pointi au njia zote au mbili au tatu nakadhalika.

Uchaguzi ni wa kwake kulingana na mazingira aliyopo. Maalumati haya yanapatikana kupitia Online au Offline kutegemea na mahitaji ya mwanafunzi.

Katika mfumo huu kuna nafasi ya mwalimu na nafasi ya mwanafunzi na hii itaelezewa katika sehemu ya pili siku chache zijazo.

Pia, upo mfumo wa kutoa mihadhara Mbashara kwa njia ya mtandao wa ZOOM na You Tube kwa wanafunzi wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Mifumo hii nayo tutaitolea makala ili Watanzania waweze kuifahamu vizuri na wajiunge na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania wapate Elimu wakiwa popote pale walipo.

Hakika hii ni fahari kubwa ya Ubunifu ambayo imefikiwa na Chuo Kikuu Huria cha Tanzania katika miaka yake 30 sasa tangu chuo kianze kutoa mafunzo na huduma kwa wananchi wa Tanzania na nje ya mipaka.

Faharasa: "Maalumati" kwa namna ilivyotumika hapa inarejelea notes au zana za kujifunza na kufundishia ambazo pia hufahamika kama "Teaching and learning resorces."

Maalumati ni neno la Kiswahili. Katika mfumo huu kuna mambo mengi, lakini leo katika sehemu hii ya kwanza tumedondoa kidogo tu na katika makala zinazofuata tutaendelea kuelezea faida za mfumo huu katika ufundishaji na ujifunzaji hapa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania.

Miaka 30 ya OUT hoyeeeeee
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania hoyeeeee
Elimu Masafa safiiiiiiiiiiiiiii
Elimu Huria safiiiiiiiiiiiiiiiiiii


MWANDISHI

Dkt. Mohamed Omary Maguo
Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Itifaki
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news