IRINGA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza miradi yote inayojengwa kwa fedha za Serikali ikamilike ndani ya mwaka huu na ianze kutoa huduma kwa wananchi.
Ametoa agizo hilo jioni ya Julai 8, 2024 wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Mwembetogwa, mjini Iringa.
Amesema uimara wa Serikali yoyote ni pamoja na uwepo wa watumishi wa umma na kupitia wao, Serikali inafuatilia mahitaji ya wananchi kwenye maeneo yote.
“Serikali yenu chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kufuatilia mahitaji ya wananchi. Katika kufuatilia, tumezihusisha Halmashauri za Wilaya kote nchini kuhakikisha kuwa zinawafikia kwenye vijiji mlipo, mnaeleza matatizo mliyonayo na wao wanaratibu kwa kuanza utatuzi wa kero zinazowagusa kwenye maeneo yenu.”
Waziri Mkuu pia alitoa fursa kwa Naibu Mawaziri na Wabunge waliokuwepo kwenye mkutano huo ambao waliambatana naye kwenye ziara ya siku nne mkoani humo ili waelezee miradi iliyotekelezwa na Serikali kwenye mkoa huo.
Mapema, akizungumza na wananchi waliohudhuria mkutano huo kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu azungumze nao, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba aliishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kupeleka fedha nyingi za miradi katika sekta mbalimbali zikiwemo za maji, afya, elimu, barabara, mawasiliano ya simu na nishati.
Akitoa mfano katika sekta ya miundombinu, Mkuu huyo wa Mkoa alizitaja baadhi ya barabara zitakazojengwa kwa kiwango cha lami zikiwemo za kutoka Ipogolo hadi Kilolo (km. 33); Mafinga - Mgololo (km. 80); mchepuo wa Mji wa Iringa, km 7.3 – (Iringa Bypass) na uboreshaji wa barabara ya Mlima Kitonga (km 7).
“Pia tumepata shilingi bilioni 50 kupitia TARURA ambapo Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini wanahudumia mtandao wa barabara nyingi za vijijini,” alisema.