Mkapa Foundation itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali-Rais Dkt.Mwinyi

NA GODFREY NNKO 

MSARIFU wa Taasisi ya Benjamin William Mkapa, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi amesema, Taasisi ya Benjamin William Mkapa itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kuchangia kuandaa nguvu kazi, kuwaendeleza na kuboresha mifumo kupitia programu ya Mkapa Fellows katika sekta ya afya.
Dkt.Mwinyi ameyasema hayo leo Julai 31, 2024 wakati wa kumbukizi ya tatu ya hayati Benjamin William Mkapa katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

"Kwa miaka michache ijayo changamoto ya nguvu kazi katika Sekta ya Afya itatatuliwa kwa kiasi kikubwa.

"Sisi katika Taasisi ya Benjamin Mkapa kwetu hii ni ajenda ya kudumu. Nitumie fursa hii kukuhakikishia kwamba Taasisi ya Mkapa itaendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuandaa nguvu kazi, kuiendeleza, kuboresha mifumo na kuchangia nguvu kazi hiyo kupitia Programu ya Mkapa Fellows tuliyonayo.

"Tutaendelea kutafuta ubunifu wa kuisaidia Serikali kuziba pengo hili, kama tulivyofanya kupitia programu ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii yaani Community Health Workers."

Ameleeza kuwa,Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatarajia kujenga Hospitali ya Rufaa ya Binguni itakayokuwa na vitanda 600 hivi karibuni.

Pia, Rais Dkt.Mwinyi amesema SMZ imetoa ajira mpya 1,050 za watumishi wa afya, imejenga jumla ya nyumba 80, ikiwa ni 16 kila wilaya zilizogharimu shilingi bilioni 20 ili kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa sekta ya afya na kuwapa motisha ya kazi.

Vilevile Rais Dkt.Mwinyi amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe.Dkt Samia Suluhu Hassan kwa juhudi anazochukua za kuboresha sekta ya afya nchini.

"Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar nayo inakabiliwa na changamoto kubwa ya nguvu kazi katika sekta ya afya.

"Changamoto hii inazidi kuwa kubwa kutokana na uwekezaji mkubwa wa miundombinu ya afya tuliyoifanya kwa kujenga jumla ya hospitali 10 za wilaya Unguja na Pemba na kujenga hospitali kubwa ya Mkoa wa Mjini Magharibi ya Lumumba yenye uwezo wa kulaza wagonjwa 208 kwa wakati mmoja na kutoa huduma za ubingwa na ubingwa bobezi.

"Hivyo, suala la afya halikwepeki kuwa suala la ushirikiano kwa ajili hiyo tunakupongeza kwa hatua unazozichukua kwa upande wa Bara, sababu pia sisi ni wanufaika wa hatua hizo."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news