NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ameelekeza Wakurugenzi wa Halmashauri wasitoke katika vituo vyao vya kazi wakati wa vikao vya Kamati ya Fedha, Bajeti pamoja na vile vya Usalama ili kusimamia kikamilifu masuala muhimu ya maamuzi na kudhibiti upatikanaji wa hati chafu katika Halmashauri.
Mhe. Mchengerwa ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kazi chake na wakuu wa wilaya wote nchini kilichofanyika katika Ukumbi wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Julius Nyerere Kibaha mkoani Pwani.
“Inaonekana sababu kubwa ya halmashauri nyingi kupata hati chafu ni kitendo cha baadhi ya Wakurugenzi kushindwa kusimamia masuala ya fedha na kutelekeza jukumu hilo kwa maafisa wa fedha na kukaimisha Ofisi kila wakato, hivyo kuanzia sasa mkurugenzi yeyote asitoke kwenye kituo chake cha kazi wakati wa vikao vya masuala ya fedha,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.
Mhe. Mchengerwa amewataka Wakuu wa Wilaya kutoa taarifa iwapo Mkurugenzi yeyote atatoka katika kituo chake cha kazi wakati wa vikao vya kujadili masuala muhimu ya mipango na bajeti vikiendelea na hasa kwenye vikao vya kamati za fedha pamoja na vya kamati za usalama.
“Katibu Mkuu sitegemei kusikia Mkurugenzi wa Halmashauri anatoka kituoni bila kumpatia taarifa Mkuu wa Wilaya kwani Mkurugenzi anapaswa kushirikiana kiutendaji na Mkuu wa Wilaya, hivyo naamini hilo halitatokea baada ya kikao hiki,” Mhe. Mchengerwa amehimiza.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amewataka Wakuu wa Wilaya hao kuzingatia mipaka ya madaraka yao kwani wao ni kiungo muhimu cha kuimarisha ushirikiano miongoni mwa viongozi na watendaji wa taasisi zote zilizopo katika ngazi ya wilaya na halmashauri.
“Katika kutekeleza majukumu yenu mnapaswa kuzingatia mipaka yenu ya utendaji kazi na hatua mtakazochukua zizingatie Kanuni, Sheria, Miongozo na Taratibu zilizopo katika Utumishi wa Umma ili mjiepushe na changamoto ya ulevi wa madaraka,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.