Mkurugenzi Mkuu wa TAEC, Prof. Najat ahitimisha ziara yake ya kikazi Kanda ya Mashariki

DAR-Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) Prof. Najat Kassim Mohammed amehitimisha ziara yake ya kikazi katika ofisi za tume, Kanda ya Mashariki jijini Dar es Salaam.
Katika ziara hiyo Prof. Najat alitembelea eneo la Mbezi-Msakuzi kuangalia maendeleo ya mradi wa ujenzi wa ofisi na maabara za TAEC ambao unajengwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa jumla ya shilingi Billioni 7.9.
Mbali na hapo pia Prof. Najat pia alitembelea Ofisi za TAEC zilizopo Bagamoyo, Mbweni na Magogoni kwenye jengo la Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (WEST) na kuongea na wafanyakazi ili kufahamu utekelezaji wa majukumu katika ofisi hizo pamoja na kusikia changamoto zinazowakabili wafanyakazi na kuahidi kuzifanyia kazi ili kuzitatua na hatimaye kuongeza ufanisi wa kazi.
Aidha, akiwa katika ziara ya Kanda ya Mashariki, Prof. Najat pia alitembelea Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI) na kukutana na uongozi wa hospitali hiyo.

Pia, Mkurugenzi Mkuu alifanya kikao cha pamoja katika kuangalia maeneo ya ushirikiano yanayohusu matumizi ya teknolojia ya nyuklia na mionzi katika uchunguzi na matibabu ya magonjwa mbalimbali.
Katika ziara hiyo Dkt. Julius Mwaiselage, Mkurugenzi Mtendaji wa Ocean Road alipokuwa akiwasilisha ripoti yake alimshukuru Prof. Najat kwa ushirikiano uliopo kati ya TAEC na ORCI, ambapo Dkt. Mwaiselage aliainisha baadhi ya mafanikio ambayo yamechangiwa na ushirikiano baina ya TAEC na ORCI kama vile uratibu wa miradi ya teknolojia ya nyuklia na mionzi.
Miradi ambayo inatekelezwa hapa nchini hususani katika sekta ya afya ambapo kupitia TAEC vifaa mbalimbali vya uchunguzi na matibabu ya mionzi sambamba na mafunzo kwa wataalam wa tiba ya mionzi yamekuwa yakitolewa na Shirika la Nguvu za Atomu Duniani (IAEA) kwa uratibu wa TAEC.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news