Mkutano wa 117 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Nchi za Afrika,Caribbean na Pasifiki (OACPS) waanza Brussels

DAR-Mkutano wa 117 wa Baraza la Mawaziri la nchi za nchi za Jumuiya ya nchi za Afrika, Caribbean na Pasifiki (OACPS) Unaofanyika kwa mfumo wa mseto kuanzia tarehe 23 hadi 26 Julai 2024 umeanza jijini Brussels, Ubelgiji.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dkt. Edwin Mhede (kushoto) akiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Bw. Msafiri Mbibo akishiriki Mkutano wa 117 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pasific unaofanyika kwa njia ya mseto ulioanza tarehe 23 Julai, 2024 jijini Brussels, Ubelgiji.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi) Dkt. Edwin Mhede , ameongoza Ujumbe wa Tanzania unaoshiriki kwa njia ya mtandao katika siku ya kwanza ya Mkutano huo ulioanza tarehe 23 Julai 2024.
Mkutano huo pia unafuatiliwa na Balozi wa Tanzania Brussels Mhe. Jestas Nyamanga na Maafisa waandamizi kutoka Wizara za Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Wizara ya Fedha, Wizara ya Viwanda na Biashara, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Wizara ya Madini, na viongozi waandamizi kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mkutano huo wa kwanza kwa mwaka huu utajadili maendeleo muhimu ya ushirikiano kati ya wanachama katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa pamoja na kuwa jukwaa la kuboresha mikakati ya kikanda na kimataifa ili kuimarisha maendeleo endelevu na ushirikiano wa kimaendeleo kati ya nchi za OACPS.

Mkutano huo pia utatoa fursa ya kuimarisha uhusiano na Umoja wa Ulaya kupitia majadiliano ya Mkataba wa Ushirikiano wa Samoa ambao unalenga kuboresha biashara uwekezaji na ushirikiano wa kisiasa kati ya nchi za OACPS na Umoja wa Ulaya.

Mkutano huo unatarajiwa kujadili na kupitisha bajeti ya OACPS kwa mwaka 2024, kupitia na kujadili taarifa za fedha za OACPS ikiwemo taarifa ya uchaguzi wa hesabu za Jumuiya, kujadili utekelezaji wa Mkataba wa Ubia kati ya OACPS na Umoja wa Ulaya kuhusu mkataba wa Samoa, kujadili taarifa ya ununuzi wa jengo jipya la Ofisi za OACPS na kujadili taarifa ya mkutano wa Mawaziri wa Madini na Nchi za OACPS uliofanyika Cameroun kuhusu uendelezaji wa madini ya kimkakati kwenye nchi wanachama.

Mkutano huo wa Baraza la Mawaziri hukutana mara mbili kwa mwaka kujadili na kuamua kuhusu masuala mbalimbali ya jumuiya na ni jukwaa muhimu kwa Mawaziri wa nchi hizo kubadilishana mawazo na kufanya maamuzi kuhusu matukio na maendeleo muhimu yaliyotokea katika kipindi cha kuanzia Juni 2023 hadi Juni 2024 ambako masuala na fursa muhimu zinazohitaji uelewa wa pamoja na mwelekeo wa kimkakati wa Mawaziri wa OACPS yalitokea.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi, Dkt. Edwin Mhede (kushoto) akiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Madini Bw. Msafiri Mbibo akishiriki Mkutano wa 117 wa Baraza la Mawaziri la Jumuiya ya Nchi za Afrika, Caribbean na Pasific unaofanyika kwa njia ya mseto ulioanza tarehe 23 Julai, 2024 jijini Brussels,Ubelgiji.
Baraza hilo la Mawaziri la OACPS linaundwa na nchi za Jamaica- Rais, Liberia- Rais anayeondoka, Jamhuri ya Kongo, Rais ajaye, Sudan- Inawakilisha Afrika Mashariki, Angola Inawakilisha Kusini mwa Afrika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo-Inawakilisha Afrika ya Kati, Burkina Faso, Inawakilisha Afrika Magharibi,Haiti Inawakilisha nchi za Karibiani na Vanuatu inawakilisha nchi za Pasifiki.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news