Msajili Mkuu wa Mahakama avutiwa na kauli mbiu ya Maonesho ya Sabasaba

NA MARY GWERA
Mahakama

MSAJILI Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya amekiri kuvutiwa na Kaulimbiu ya Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba kwa kuwa, Mahakama nayo ina mchango katika kuwezesha mazingira ya biashara na uwekezaji.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (aliyesimama katikati mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na Wadau wanaotoa elimu katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), 2024 yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Temeke jijini Dar es Salaam. Mhe. Nkya ametembelea Maonesho hayo tarehe 10 Julai, 2024.

Mhe. Nkya ameyasema hayo tarehe 10 Julai, 2024 mara baada ya ziara yake ya kutembelea Maonesho hayo yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Temeke jijini Dar es Salaam.

“Nimevutiwa na maonesho yenyewe lakini pia kaulimbiu ya mwaka huu ambayo inatuambia kwamba Tanzania ni mahali sahihi pa biashara na uwekezaji, kaulimbiu hii ukiiunganisha na Mahakama kwenye shughuli za Mahakama inawezekana migogoro ikawepo, kwa hiyo na sisi kama Mahakama ni kuhakikisha kuwa tunaweka mazingira ya utatuzi wa migogoro,” amesema Msajili Mkuu.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Wizara ya Katiba na Sheria wanaotoa msaada wa sheria katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba) yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Temeke jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa, ili kuwa na mazingira wezeshi ya kiuwekezaji kwa Nchi, Mahakama Kuu ya Tanzania iliona ni vema kuanzisha Divisheni ya Biashara ili kushughulikia mashauri/ migogoro ya kibiashara kwa lengo la kushughulikia mashauri ya aina hiyo.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya akisaini kitabu cha wageni alipowasili katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kwa ajili ya kutembelea Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), 2024 yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa Temeke jijini Dar es Salaam.

Amesema kuwa, lengo la uwepo wa Mahakama katika Maonesho hayo ni pamoja na kuelimisha wadaawa na wananchi kwa ujumla kuhusu masuala mbalimbali ya Mahakama na sheria kwa ujumla ikiwemo taratibu za ufunguaji wa mashauri.

“Sisi kama Mahakama ambao tumepewa dhamana ya kufanya utatuzi wa migogoro tuko hapa kwa ajili ya kutoa huduma ambazo tunazifanya mahakamani, kuelimisha wadaawa na wananchi kwa ujumla ni kwa jinsi gani ambavyo shughuli ya usikilizaji wa mashauri inafanyika na hii yote ni kwa ajili ya kuleta ustawi wa jamii lakini pia kuifanya Tanzania kuwa mahali sahihi pa biashara na uwekezaji,” amesema Mhe. Nkya.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Kiaki Nkya (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Maafisa wa Mahakama na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) alipotembelea katika Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), 2024 tarehe 10 Julai, 2024.

Msajili huyo ameeleza kuwa, Mahakama inafanya maboresho mbalimbali yanayolenga kuhakikisha kuwa, huduma ya haki inapatikana kwa wakati kama ilivyo Dira yake, ametaja jitihada kadhaa zimechukuliwa na Mhimili huo nazo ni pamoja na uanzishwaji wa mifumo mbalimbali ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ya kurahisisha upatikanaji wa haki, uanzishwaji wa Kituo cha Huduma kwa Mteja (Call Centre), uanzishwaji wa Mahakama Inayotembea na kadhalika.

Aidha, Mhe. Nkya amewakumbusha wananchi kuendelea kutoa malalamiko, maoni na pongezi ili Mahakama iendelee kufanyia kazi maeneo yenye mapungufu kufuatia mirejesho inayotolewana wananchi.

Amewakumbusha kupiga namba ya bure ya 0800750247 na namba ya Huduma kwa Mteja ya 0752 500 400 ili kutoa malalamiko, maoni na hata pongezi.
Picha za juu, Msajili Mkuu akiwa katika mabanda mbalimbali yaliyopo ndani ya banda la Mahakama ya Tanzania katika Maonesho ya Sabasaba yanayoendelea kufanyika katika Viwanja vya Mwalimu Nyerere barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.
Ametoa wito kwa wananchi kutembelea banda la Mahakama ya Tanzania na mabanda mengi ili kufahamu taratibu na huduma zinazotolewa na Mahakama pamoja fursa nyingine za biashara na uwekezaji kwa ustawi jamii na Nchi.

Mahakama ya Tanzania inaendelea kutoa huduma zake katika Maonesho hayo ambayo yatafikia tamati Jumamosi tarehe 13 Julai, 2024.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news