MBEYA-Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya imewahukumu Kaimu Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Kimondo, Mwenyekiti wa Kamati ya Pembejeo za Kilimo katika Kijiji cha Kimondo na Wakala wa Pembejeo wa Kampuni ya Highlands Seed Growers Limited kwa kughushi nyaraka.
Aidha, washtakiwa hao wametakiwa kulipa faini ya shilingi milioni 1.3 kwa kila mmoja au kwenda jela miaka minne iwapo watashindwa kulipa faini hiyo.
Hukumu hiyo imetolewa baada ya kila mmoja kukutwa na hatia kwa kosa la kwanza hadi la tisa linalohusu matumizi ya nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri na kwa kosa la 10 hadi 17.
Makosa hayo ni kinyume na kifungu cha 22 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11/2007 na kughushi kinyume na vifungu vya 333, 335 na 337 vya Kanuni ya Adhabu. (CAP 16 RE 2022).
Hukumu hiyo imetokana na shauri la jinai Na. 11/2023 iliyosomwa Julai 3, 2024 na Hakimu Mkazi Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya Mtengeti Sangiwa.
Washtakiwa walifikishwa mahakamani kwa mashtaka ya kutumia nyaraka kwa lengo la kumdanganya mwajiri na kughushi nyaraka katika zoezi la ugawaji wa pembejeo za kilimo msimu wa 2015/2016.Hata hivyo ,Washtakiwa wamelipa faini na kuachiwa huru