Mwinjilisti Temba akosoa kauli ya CPA Makalla

DAR-Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa, Alphonce Temba ameibuka na kuhoji kauli ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), CPA Amos Makalla kuhusiana na hoja yake aloyoitoa hivi karibuni kwamba CCM italeta wagombea wenye kiu ya kutatua kero.
Temba amesema, kwa sasa wanahitajika viongozi ambao wanaweza kudhibiti mianya ya rushwa, kwa sababu adui mkubwa wa Serikali na maendeleo ya Taifa lolote ni rushwa na wizi.

Ameibuka baada ya kauli hiyo na kuikosoa kwa kusema kwamba, Chama Cha Mapinduzi hakihitaji viongozi watakaosaidia kutatua kero kwa Watanzania.

"Kwa sababu, kama kitahitaji viongozi wa kusababisha kutatua kero nchini, basi italazimika kujua hizo kero zinatengenezwa upande gani, na zinatatuliwa upande gani na kwa nini kero zitengenezwe na kwa nini kero zisiwepo."

Hivyo, amemshauri CPA Makalla kwamba anapaswa kutambua huu ni wakati wa Sayansi na Teknolojia ambapo umma unafahamu kila kitu kinachoendelea.

"Na tumeona Taifa pia la Tanzania limeanza kuwekeza katika Akili Mnemba (AI) kutokana na teknolojia.

"Tayari tumeona, Serikali ikitambulisha roboti Eunice kule bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari , Mheshimiwa Nape Nnauye (Mb).

"Pia, tumeona roboti ambayo ni akili mnemba ikiwepo katika Maonesho ya ya Biashara ya Kimataifa jijini Dar es Salaam (Sabasaba) na wananchi wamekuwa wakifanya mazungumzo nayo.

"Na kuona namna ambavyo Taifa linakwenda kwa kasi, na Mama yetu, Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amekusudia kabisa twende na kasi ya teknolojia kwa ustawi bora wa uchumi wa kidigitali.

"Hivyo, neno la CPA Amos Makalla lina ukakasi sana, kwamba wananchi wana teknolojia ya juu sana, halafu bado kuna maeneo wanarudishwa mwaka 47. Viongozi wa kutatua kero, wakati wake umepita hiyo ni miaka ya 60 huko, miaka ya 70 baada ya Uhuru.

"Sasa hivi tunahitaji viongozi ambao wanaweza kudhibiti mianya ya rushwa, kwa sababu adui mkubwa wa Serikali, adui mkubwa wa mapato ya nchi, adui mkubwa wa jamii ni rushwa na wizi ambao bado umeonekana kutokana na taarifa mbalimbali za Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

"Kuna mianya michache iliyobaki ya ya rushwa na upigaji. Upigaji huo ni mkubwa katika miradi mbalimbali iwe ya shule, hospitali, iwe ya halmashauri na iwe miradi mbalimbali ya biashara nchini kumekuwa na upigaji mkubwa ndani na nje ya nchi ukiangalia katika balozi zetu kuna upigaji.

"Kwa hiyo sasa hivi, tunahitaji katika kila eneo, kila sekta ambayo wanakuwa na mamlaka nayo waweze kudhibiti, wawe ni viongozi wanaochukukia rushwa.

"Wawe ni viongozi ambao wanaopambana na ile keki ya Taifa ili iweze kuendelea kwa sababu hata Mheshimiwa Rais anavyopambania kuhusiana na mapato yapatikane.

"Tumeona taarifa mbalimbali, tumeona mabadiliko Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili uweze kuwepo umakini wa ukusanyaji wa mapato uwe mkubwa na Tanzania imekuwa ikifanya kazi kubwa.

"Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan amepambana kwa nguvu kubwa, tumeona akibadilisha watendaji, akibadilisha mawaziri, akivunja kamati mbalimbali, akivunja bodi mbalimbali hii yote ni kwa sababu ya kupata kipato cha kuendesha nchi.

"Lakini, bado udhibiti wa fedha zinazopatikana katika mkono wa Serikali ndiko kuna kansa na shida na ndiko sasa CCM inatakiwa ituletee viongozi ambao watakwenda kuitatua hiyo kansa ya wizi wa fedha hasa za miradi za Serikali na kadhalika ambayo taarifa zake zipo kamili katika ripoti ya CAG kila mwaka tukiona wizi, upotevu mkubwa, kamati za Bunge mbalimbali zimekuwa zikilalamika na kuelezea taarifa za Bunge.

"Hansard za Bunge zipo nyingi zinazoonesha wizi katika taasisi mbalimbali, wakurugenzi kadha wa kadha, wengine wamepelekwa mahakamani. Kesi zipo mahakamani ufujaji wa fedha, upigaji mkubwa katika maeneo mbalimbali huku miradi mingine ikijengwa chini ya viwango."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news