SHINYANGA-Naibu Waziri wa Nishati. Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali inaendelea kuwasimamia kwa umakini wakandarasi ili waweze kukamilisha kazi zao kwa wakati na kwa ufanisi, pia amewaelekeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhakikisha wanaongeza nguzo 40 ambazo ni Sawa na kilometa mbili kwa wananchi wa vijiji vya Manzwagi na Kidunyashi kabla ya tarehe 27 Julai, 2024.
Mhe. Kapinga amesema hayo Julai 3, 2024 alipokuwa anahitimisha ziara yake katika Wilaya ya Kahama kwenye Vijiji vya Manzwagi na Kidunyashi vilivyopo Wilaya ya Kahama Mjini mkoani Shinyanga.


Amesema kutokana na suala la maendeleo kuwa ni hatua, Serikali iliweka nguvu kubwa katika usambazaji wa umeme vijijini na sasa hatua inayofuata ni kupeleka umeme vitongojini ili kuwezesha shughuli za kijamii na kiuchumi.
"Nawashukuru REA wamesema watawafikishia umeme watu wa Manzwagi tarehe 14 julai 2024 niwatowe hofu wananchi wa Manzwagi kuwa umeme utawafikia Ndani ya siku zilizopangwa na pia tutawaongozea Nguzo nyingine 40 ili umeme uweze kufika vijiji vyote," amesema Kapinga.

"Mradi mkubwa wa Julius Nyerere (JNHPP) unaozalisha Megawati 2.115 umegharimu zaidi ya trilioni 6 ambapo mradi huu mkubwa utatufanya tuweze kuzalisha umeme zaidi ya huu tunaoutumia sasa," ameeleza Kapinga.
Naibu Waziri Kapinga ametoa wito kwa Wananchi kuhakikisha wanailinda miundombinu ya umeme ili iweze kutumika kwa muda mrefu.
"Niwaombe Wananchi tutunze miundombinu hii ya umeme ili iweze kutumika kwa muda mrefu pamoja na kutuletea tija katika shughuli zetu za Maendeleo,"amesisitiza Kapinga.
Aidha kuhusu bei ya umeme, Mhe. Kapinga ameongeza kuwa atakaa na REA na kufanya tathimini bei ya kuunganisha ya 320,000 au 27,000.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Mhe. Julius Mtatiro ameshukuru kazi kubwa ya usambazaji umeme inayofanywa katika maeneo mbalimbali na pia amempongeza Mbunge wa Kahama Mjini Mhe. Jumanne Kishimba kwa kuwajali wananchi kwa kuwapatia Maendeleo kwa wakati.