Nenda kajenge nyumbani…Mtaka anawaita

NA LWAGA MWAMBANDE 

WATAALAMU wa masuala ya makazi wamekuwa wakibainisha kuwa, kumiliki nyumba yako ni mafanikio makubwa sana si kwako tu bali kifamilia.
Kwani, kuanzia watoto mpaka mwenza wako wataongeza imani na heshima kwako na hata wao watajihisi wamekamilika zaidi kisaikolojia kwa kuwa na nyumba bora.

Pia,kumiliki nyumba yako kunakupa fursa kulea watoto katika malezi sahihi na ambayo unayahitaji.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa,malezi ya siku hizi yamekuwa ni changamoto sana kutokana na utandawazi na ukisasa ambao kwa sehemu kubwa unaleta uharibifu mkubwa hasa kwa watoto ambao bado hawajajua lipi la kufanya na lipi la kuacha katika maisha ya kila siku.

Vivyo hivyo, utaweza kuwa na udhibiti sahihi wa malezi kwa watoto na kuepuka kusaidiwa malezi na watu waliokosa maadili kijamii.
Ujenzi wa makazi miaka ya karibuni umeendelea kuwa rahisi si tu kwa upande wa mijini, lakini pia huko vijijini kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo imefanikishwa na Serikali.

Utekelezaji huo mfano miundombinu ya barabara, nishati na nyinginezo zimekuwa kivutio kwa wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi, hivyo kila unachohitaji kwa ajili ya ujenzi utakipata popote ulipo.

Mshairi wa kisasa kwa kutambua umuhimu wa kila mtu kujenga makazi (nyumba), amerejea wito wa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mheshimiwa Anthony Mtaka kuhusu umuhimu wa kwenda kujenga nyumbani. Endelea;

1.Nenda kajenge nyumbani, Njombe mnaitwa huko,
Mliko ni ugenini, jijenge kwenu na huko,
Msibakie mjini, nyumbani nyumba haiku,
Mtaka anawaita, hebu kuwa na busara.

2.Ni Mkuu wa Mkoa, anayewaita huko,
Anaona mnaboa, kutejenga nyumba huko,
Mjini mnasogoa, kuwekeza vyote huko,
Mtaka anawaita, hebu kuwa na busara.

3.Nyumbani si kaburini, bila ya nyumba kuweko,
Sikia jitahidini, kaweke mijengo huko,
Mjini na vijijini, nyumba ziwe za mashiko,
Mtaka anawaita, hebu kuwa na busara.

4.Matukio yatokea, hayafurahishi huko,
Msiba ukitokea, magari ya ghali huko,
Watu wameendelea, nyumbani nyumba haziko,
Mtaka anawaita, hebu kuwa na busara.

5.Ni maendeleo Njombe, kuna kila kitu huko,
Barabara nzuri Njombe, kufika Makete huko,
Ludewa nako mtambe, mambo mema mengi huko,
Mtaka anawaita, hebu kuwa na busara.

6.Enyi wenyeji wa Njombe, igeni wenzenu huko,
Mjini nyumba mtambe, pia na kwenu ziweko,
Likizo muende Njombe, watoto wajue huko,
Mtaka anawaita, hebu kuwa na busara.

7.Mambo ya uchawichawi, yalikuweko hayako,
Viatu pigeni kiwi, kwa raha nendeni huko,
Nyumbani kukastawi, miradi peleka huko,
Mtaka anawaita, hebu kuwa na busara.

8.Mungu amewajalia, mnao watoto huko,
Msiache waambia, asili yao iliko,
Likizo ikiingia, hebu wapeleke huko,
Mtaka anawaita, hebu kuwa na busara.

9.Ujumbe sio wa Njombe, unahusu kwingineko,
Kote uliko utambe, nyumbani nyumba iweko,
Si kusubiri tuimbe, kifo na nyumba haiku,
Mtaka anawaita, hebu kuwa na busara.

10.Amewataja Wachaga, jinsi wanafanya huko,
Mjini wanazo swaga, nyumba nzurinzuri huko,
Kwenda kwao wakiaga, mijengo ni mingi nako,
Mtaka anawaita, hebu kuwa na busara.

Lwaga Mwambande (KiMPAB)
lwagha@gmail.com 0767223602

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news