NA JAMES MWANAMYOTO
OR-TAMISEMI
NAIBU-Waziri, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Elimu) Mhe. Zainab Katimba amesema, amefurahi kuona shule mpya ya maalum ya wasichana ya mkoa wa Kigoma imepokea wanafunzi kama ilivyokusudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mhe. Katimba ameshuhudia wanafunzi wakiwa katika shule hiyo maalum ya wasichana ya mkoa wa Kigoma, alipoitembelea kwa lengo la kujiridhisha na kiwango cha ujenzi wa shule hiyo ambayo imejengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza.
Mhe. Katimba amesema, Rais Samia alitafuta fedha za kujenga shule maalum za sayansi za wasichana kila mkoa ili kuwawezesha kupata miundombinu bora itakayokuwa chachu kwa watoto wa kike kusoma masomo ya sayansi.
“Wanasayansi wetu wa kesho si mmeona jitihada za Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhakikisha amewajengea shule nzuri hivyo jukumu lenu kubwa ni kuhakikisha mnasoma kwa bidii,” Mhe. Katimba amewaasa wanafunzi wa shule hiyo.
Mhe. Katimba amewataka wanafunzi hao kuzingatia masomo ili wamalize shule salama na baadae wawe na maisha bora yaliyochagizwa na miundombinu bora ya elimu ambayo imejengwa na Rais Samia ambaye tangu aingie madarakani alidhamiria kuwapatia fursa watoto wa kike ya kupata elimu bora.