Nishati safi ya kupikia yashika kasi, Serikali yaahidi jambo kubwa kwa wananchi

RUVUMA-Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika mwaka huu wa fedha itatoa mitungi ya gesi takriban 400,000 kwa wananchi yenye thamani ya shilingi bilioni kumi. Akizungumza na wananchi wiilayani Mbinga leo tarehe 23 Julai 2024, Mhe. Kapinga amesema lengo la Serikali ni kuongeza matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia nchini kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira na kuwaepusha wananchi na maradhi yanayotokana na matumizi ya nishati isiyo safi.
"Hadi sasa kupitia REA tumeshatoa mitungi ya ruzuku 83,500 yenye thamani ya shilingi bilioni 3.5 na kazi inaendelea,"amesema Mhe.Kapinga

Ameongeza kuwa, nia ya Serikali ni kupunguza gharama za vifaa vya nishati safi ya kupikia ili wananchi wapate huduma kwa bei nafuu.

Amesisitiza kuwa, Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na wadau ili kuongeza Mawakala hadi ngazi ya Vijiji ikiwemo kutoa ruzuku kwa mawakala hao kupitia miradi mbalimbali.
Mhe. Kapinga amesema kutokana na jitihada zinazofanywa na Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan katika nishati hiyo, Tanzania imeonekana kuwa kinara wa utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia kupitia Sera mbalimbali na Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya kupikia wa 2024 hadi 2034.
"Sio siri Mheshimiwa Rais ndiye aliyeleta hamasa kubwa sana ya matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na hii inaiweka Tanzania kama kinara wa Ajenda hii duniani."

Kwa upande wake, Kaimu Meneja Msaidizi Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka REA, Mhandisi Emmanuel Yesaya amesema kazi ya Wakala wa Nishati Vijijini ni kuhamasisha na kufadhili miradi ya nishati vijijini pamoja na kujenga uwezo kwa Wawekezaji miradi na kuhamasisha utunzaji wa mazingira kupitia miradi ya nishati safi ya kupikia.
Ameongeza kuwa, nishati safi ya kupikia inapimwa kwa ufanisi, upatikanaji, usalama, urahisi wa kuitumia na pia isiyomweka mtumiaji kwenye mazingira hatarishi yenye sumu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news